Amuua mpenzi wake baada ya kumfumania akimeza arv kisiri siri

Dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi


Mwanamke mmoja katika wilaya ya Hoima Mashariki mwa Uganda anashikiliwa
kwa madai ya kumuua mpenzi wake baada ya kumfuma akimeza dawa za
kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV).
Polisi wamesema siku ya Alhamisi kuwa Emmanuel Tumusiime, 35
alishambuliwa mpaka kuuawa katika makazi yake akiwa mji wa Kigorobya
majira ya saa kumi na mbili jioni siku ya Jumatano.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor nchini Uganda, msemaji wa polisi
wa mji huo, Bwana Julius Hakiza amesema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa
Tumusiime alipigwa kichwani na shoka.
”Alipogundua kwamba mpenzi wake amefariki, mshukiwa alifunga nyumba na
kupanda Bodaboda mpaka kwenye kituo kikuu cha polisi cha Hoima na
kuripoti kesi ya mauaji,” alieleza Bw. Hakiza.
Katika kituo hicho cha polisi, mwanamke huyo alikiri kumuua mpenzi wake.
Mwanamke huyo anadai kuwa alijisikia uchungu sana baada ya kuhisi kuwa kuna uwezekano ameambukizwa virusi vya Ukimwi.
Alikamatwa na kushikiliwa kwenye kituo kikubwa cha Hoima akishutumiwa kwa kujihusisha na mauaji.
Wapelelezi walikimbilia eneo la tukio na kulifunga kwa ajili ya uchunguzi zaidi, alieleza Hakiza.
”Tunatoa wito kwa waathirika wa virusi vya Ukimwi mara zote kuwapa
taarifa wenza wao na kuhudhuria vituo vya ushauri nasaha na kufahamu
kwamba kwa kuwa mwathirika, haimaanishi ni mwisho wa maisha,” alishauri
Hakiza.
Chanzo -BBC