Atakayefichua wakwepa kodi atalipwa asilimia 3 ya kodi itakayokombolewa



Na Veronica Kazimoto

Meneja
wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana
Masalla amesema kuwa, mwananchi yeyote atakayefichua wakwepa kodi na TRA
ikafuatilia na hatimaye kodi hiyo ikagundulika ni kweli ilikuwa
imekwepwa na ikakusanywa, mwananchi aliyetoa taarifa hizo za ukwepaji
kodi atalipwa asimilia 3 ya kodi iliyokusanywa lakini haitazidi shilingi
milioni 20.

Masalla
ameyasema hayo wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika
katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambalo lengo lake ni kujadili
fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na
wawekezaji wilayani humo na kuzitafutia ufumbuzi.
“Natoa
wito kwa wananchi na washiriki wa jukwaa hili kuhakikisha mnawafichua
wakwepa kodi wote kwa sababu watu hao wanaiibia Serikali yetu mapato na
wanarudisha nyumba jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi
wake,” Amesema Masalla.
Aidha,
Masalla amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki jukwaa
hilo kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa pindi wanapokuwa wamefunga
biashara kutokana na sababu mbalimbali ili kuepuka kuendelea kutozwa
kodi au kuonekana wamekaidi kulipa kodi.
“Ni
muhimu kutoa taarifa TRA pale ambapo mfanyabiashara amefunga biashara
yake lakini pale anapofungua ni muhimu pia kuitaarifu TRA ili kuepuka
kuendelea kutozwa kodi unapofunga biashara na pia kuanza kutozwa kodi
sahihi pale unapofungua biashara,” amesisitiza Masalla.
Naye,
Mwenyekiti wa wafanyabiashara Wilaya ya Busega David Mateko amempongeza
Meneja wa TRA Mkoa wa Simuyu kwa kutoa elimu ya kodi kwa makundi
mbalimbali ya wafanyabiashara mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo
kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na hatimaye
kuifanya Wilaya ya Busega kuwa wilaya ya pili kati ya wilaya 5 za mkoani
Simiyu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayosimamiwa na TRA.
“Nampongeza
Meneja wa TRA katika Mkoa wetu wa Simiyu kwa kuwatembelea
wafanyabiashara na kuwapatia elimu ya kodi na pia nachukua fursa hii
kumpongeza Mkuu wetu wa Wilaya Mheshimiwa Tano Mwera kwa kutuhamasisha
kulipa kodi kwa wakati na sasa wilaya yetu imekuwa ya pili hapa mkoani
kwa ukusanyaji Mapato yanayosimamiwa na TRA,” alibainisha Mateko.

Jukwaa
hili la biashara na uchumi wilayani Busega limewakutanisha
wafanyabiashara na wawekazaji zaidi ya 200 ambapo taasisi mbalimbali za
Serikali zimealikwa kutoa mada ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato
Tanzania