Egidia Vedasto, APC Media, Arusha.
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamehimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya Tehama ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia Duniani sambamba na kuimarisha ushirikiano wa utendaji kazi baina TFS na Taasisi zingine Nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi na Makanda wa Wakala wa Misitu Nchini ambacho hufanyika kila mwaka, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema matumizi bora ya Tehama yakizingatiwa mapato yataongezeka, kukomeshwa kwa rushwa lakini pia ushirikiano kiutendaji kutokana na kusomana kwa mifumo.
“Ndugu zangu wa TFS nyie ni mashahidi kwamba teknolojia imefanya mageuzi makubwa katika kazi zetu, licha ya kuturahisishia kazi, inaimarisha usalama, kufanya mifumo kusomana na kufanya kazi kama timu mfano Wizara, TRA na EGa” amefafanua Balozi Chana.
Aidha amesisitiza matumizi ya Satelaiti, na ndege nyuki (drons) katika kukabiliana na uharibifu wa misitu pale kunapotokea mioto misituni, pia kufikiria kununua vifaa vya kurahisisha utendaji kama Ndege, Helikopita na vinginevyo kutokana na kupanda kwa mapato ambayo yamefikia Bilioni 221.6.
Balozi Dkt. Chana amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya Watumishi ikiwemo kuongeza mishahara, kuwapandisha madaraja na kumaliza changamoto zingine, kuongeza vituo vya ulinzi, na kuwataka kutumia mbinu za kijeshi kazini, katika namna hiyo hiyo amewahimiza kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia misingi ya maadili kama inavyoelekeza ili kuongeza pato la Taifa na kufikia malengo.
“Nawapongeza TFS kwa namna ambavyo mmekuwa mkishirikiana na Wananchi ngazi za Vijiji, kutoa miche ya misitu bure naelekeza utaratibu huo uendelezwe katika Shule za Msingi na Sekondari, Magereza, na katika Taasisi zingine
ili kuongeza wingi wa miti itakayosaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mvua na kuongeza mavuno ya chakula na asali” amefafanua Balozi Dkt. Chana.
Kwa upande wake Kamishna wa Wakala wa Misitu Nchini Profesa Dosantos Silayo amesema Kikao hicho kilichojumuisha Makanda takriban 240 kinakusudia kujadili mafanikio na changamoto katika sekta ya Misitu nchini na masuala ya maadili na uadilifu kwa watumishi wa TFS.
“Katika kikao hiki tutajiwekea maazimio yetu ya kazi, kukumbushana wajibu na kuimarisha misingi ya utendaji, katika kufanikisha hayo yote tumealika watoa mada mbalimbali ili kutoa elimu na miongozo mbalimbali itakayoboresha utendaji kazi wetu” ameeleza na kuongeza
“Mkutano huu wa Makamanda wa TFS umeenda sambamba na Bonanza lililofanyika Jijini Arusha kutoka kanda nane, lililokusudia kujenga ushirikiano baina ya watumishi na kuimarisha afya ya akili” amesema Profesa Silayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya TFS aliyewakilishwa na Eng. Emmanuel Nyanda amesema, Taasisi imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa weledi ikiwemo watumishi kupandishwa madaraja kutokana na sifa zao.
“Asilimia 95% ya Makamanda wote nchini wamepata mafunzo ya kijeshi na utayari, wana imani na furaha juu ya Bodi hii, pia kufikia Juni 2024 TFS imekamilisha ujenzi wa majengo 20 na Bodi inaomba uyafungue ili yatumike kama ilivyokusudiwa” ameeleza Eng. Nyanda.
Ameeleza kuwa, Bodi itaendelea kusimamia na kuboresha vifaa na rasilimali, kubuni vyanzo vipya vya mapato kwani idadi ya misitu iliyopo haiendani na mapato ya sasa.
Pia katika mafanikio Bodi inajivunia kutatua migogoro kwa asilimia 96% ambapo imetatuliwa migogoro 423 kati ya 435.
Akizungumza katika Mkutano huo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Arusha, Afisa Kilimo Mkoa Daniel Lairuck amesema, Ofisi ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano katika mikutano mingine inayotarajiwa Jijini humo sambamba na hayo amesema wataendelea kupambana na watu wachache na tassisi wenye nia ya kuharibu kile kinachotengenezwa.
“Kama inavyofahamika Arusha ni kitovu cha utalii nchini, na utalii unategemea asili na mazingira yote, ambayo TFS wanafanya vizuri kuonyesha jitihada za kuipa Nchi na Mkoa heshima, ustahimilivu wa ikolojia na utalii” amesema Lairuck.
Hata hivyo ameiomba TFS kuweka miundombinu ya kupumzikia katika maeneo ya utalii na uchumi mfano Ziwa Duruti na Shamba la Miti la Meru, na kuomba maeneo haya yaendelee kutangazwa, kulinda vyanzo vya maji, kulinda miti na misitu iliyopo na kuhamasisha upandaji upya miti, hatua itakayofanya nchi kuwa kinara katika zao la ufugaji nyuki.