Balozi iddi: taasisi ziboreshe mifumo ya kukusanya mapato ya serikali




Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akisikiliza kwa makini
maelezo ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Dkt. Gabriel Mukungu
kuhusu namna watuhumiwa wa makosa barabarani wanaokamatwa kwa kutumia
Mfumo wa Usimamizi wa Makosa Barabarani (TMS) wanavyolipia faini zao kwa
kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Maduhuli ya Serikali (GePG)
katika banda la Serikali  kwenye Mkutano wa Mawaziri Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya
Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa, Jijini Dar es Salaam.



Na Farida Ramadhani, WFM, Dar es Salaam



Taasisi za Serikali zinazotumia mifumo
ya kielektroniki zametakiwa kuhakikisha zinaanzisha mfumo wa kuziwezesha
kuona taarifa za kila taasisi pindi watakapo huisha mifumo hiyo.



Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili
wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi
alipotembelea banda la Serikali Na. 26 la mifumo ya kielektroniki ya
kukusanya maduhuli ya Serikali (GePG), Mfumo wa Usimamizi wa Makosa
Barabarani (TMS) na Mfumo wa Taarifa za Mali zilizopote (Los Report
System) katika Mkutano wa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama
wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama,
Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa.



Balozi Iddi ambaye alifunga mkutano huo,
alisema kitendo cha taasisi kuweza kuona taarifa kutoka taasisi
nyingine kutarahisisha kazi na kuongeza ufanisi wa Serikali katika
kuhudumia wananchi.



“Kama GePG inarahisisha malipo kwa
taasisi zote ni vema kukawa na mfumo wa kuziwezesha taasisi hizo hasa
zinazotegemeana kuweza kushirikishana taarifa, kama mtu akienda TRA
kuhuisha leseni na anadaiwa na Trafiki basi mfumo uoneshe kuwa anadaiwa
moja kwa moja”, alisema.



Aidha Balozi Iddi alipongeza mifumo ya
GePG, TMS na ule wa taarifa za mali zilopotea na kusema kuwa mifumo hiyo
ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na imeanzishwa wakati muafaka.



Alisema kuwepo kwa mifumo hii kunaiwezesha Serikali kupata mapato ya kuendeleza miradi mabalimbali ya maendeleo.



Akizungumzia mfumo wa GePG Mkuu wa
Uendeshaji wa Mfumo huo, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Basil
Baligumya, alisema mfumo umeunganisha taasisi zote za Serikali ambapo
kila malipo ya taasisi hizo hupitia katika mfumo huo.



Alisema mfumo huo umeongeza makusanyo
ya Serikali, umedhibiti fedha za umma, umeongeza uwazi katika ukusanyaji
wa mapato ya Serikali, pamoja na kuongeza usahihi wa taarifa za mapato.



Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi, Dkt. Gabriel Mukungu alisema kuwa mfumo wa TMS unasaidia
kudhibiti makosa ya barabarani kwa kuwakamata wahalifu wote wa makosa
hayo kwa kuwa mfumo huo unawezesha kuona watu wote wanaodaiwa tozo za
makosa barabarani.