Balozi seif akemea uharibifu wa mazingira zanzibar.

Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
Wananchi wa Kijiji cha Kitope Mbaleni mara baada ya kuutembelea Mradi wa
Ujenzi wa Tangi la Maji safi na salama Kijiji hapo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
amesema Visiwa vya Zanzibar vinaweza kupata mtikisiko mkubwa wa uchafuzi
wa Mazingira iwapo Watu wataendelea kuchimba Mchanga kiholela pamoja na
matumizi yasiyo  na Mpango  ya Rasilmali za Mawe.


Amesema Serikali imelazimika kuandaa utaratibu maalum wa upatikanaji
wa Rasilmali hizo muhimu katika harakati za Ujenzi wa Majengo na
Miundombinu mbali mbali kufuatia athari kubwa iliyokwishajitokeza kwenye
mashimo ya mchanga ambayo baadhi yake huchipuka maji ya chumvi.


Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo mapema asubuhi alipofanya
ziara fupi ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Tangi kubwa la Kuhifadhia Maji
safi na salama katika Mtaa wa Kitope Mbaleni baada ujenzi wake kusua sua
kutokana na ukosefu wa nyenzo za kutekeleza Mradi huo ikiwemo Mchanga,
Kokoto na Mawe.


Amesema Nchi hivi sasa imeharibika kutokana na mashimo mengi
yaliyochimbwa kwa ajili ya kupata Mchanga wa Ujenzi hali inayoashiria
lazima zipatikane mbinu mbadala za kukabiliana na changamoto hiyo ya
uchafuzi wa Kimazingira inayoweza kuleta maafa hapo baadae.


Balozi Seiif amefahamisha kwamba Serikali kwa kushirikiana na
Washirika wa Maendeleo, Wataalamu, Taasisi pamoja na Jumuiya za Kiraia
zinafanya jitihada za makusudi katika kuona Ujenzi utakaobuniwa wa
Majengo ya Taasisi za Umma na Binafsi yanazingatia mfumo wa kutumia
Mchanga kidogo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Taasisi ya Kiraia ya
Tanzania Youth Icon {TYI} pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA}
kupitia Wadau wao wa Maendleo kwa uwamuzi wao wa Kujenga Tangi hilo
litakalofaidisha Wananchi waliomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.


Alisema Kitope ni eneo lenye usumbufu wa huduma za Maji safi na
salama kwa muda mrefu tokea kuharibika kwa Tangi la zamani la kuhifadhia
Maji na Wananchi wanaozunguuka eneo hilo wamekuwa wakipata changamoto
ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu kwa ustawi wao.


Mapema Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Tangi hilo la kuhifadhia
Maji safi na salama Kitope Mbaleni Bwana Jackson Maro alimueleza Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Tangi hilo litakapokamilika litakuwa
na uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya Lita 50,000.


Mhandisi Maro alisema kazi hiyo imeanza rasmi kwa hatua ya msingi
karibu Wiki Tatu sasa, lakini imeshindwa kuendelea kama ilivyopangwa
kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa wakati wa Rasilmali ya Mchanga,
Kokoto pamoja na Mawe.


Naye Mwakilishi wa Taasisi ya Kiraia ya Tanzania Youth Icon {TYI}
Bwana Abdullah Miraji Othman alisema juhudi zimefanywa na Taasisi yake
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar{ ZAWA} za kuandika Barua
katika Taasisi zinazosimamia Rasilmali zisizorejesheka lakini bado
upatikanaji wa Rasilmali hizo umekuwa mdogo.


Bwana Miraji alitahadharisha kwamba Mradi wa Ujenzi huo umepangwa
kukamilika ifikapo Tarehe 31 Disemba Mwaka huu vyenginevyo Wafadhili
waliojitolea kuwezesha Mradi wa Ujenzi huo  wataondoa Fedha zote
walizozitenga.