Bosi shule za zam zam akutwa amefariki ofisini kwake

Mkurugenzi wa Shule za Zam Zam jijini Dodoma nchini Tanzania, Sheikh
Rashid Bura amekutwa amefariki dunia ofisini kwake eneo la Majani ya
Chai karibu na Nyerere square jijini Dodoma.
Bura aliondoka nyumbani kwake zaidi ya siku nne zilizopita na
hakujulikani alipokwenda ambapo juhudi za kumtafuta zilifanyika bila
mafanikio hadi jana Jumatano Desemba 25, 2019 alipokutwa ofisi kwake
akiwa amekufa huku mlango wa ofisi ukiwa umefungwa.
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu alikiri kuwapo kwa kifo hicho
lakini akasema wasemaji ni Jeshi la Polisi huku akisema katika imani ya
dini ya Kiislamu kifo kinaweza kumkuta mwanadamu mahali popote.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto hakuwa tayari
kuzungumzia tukio hilo lakini alikuwapo wakati mwili huo unachukuliwa
jana Jumatano saa moja jioni ukapelekwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa
ya Dodoma.
Msiba uko nyumbani kwake Mtaa wa Chang’ombe jijini Dodoma.