Breaking news: benard membe afukuzwa uanachama ccm….makamba asamehewa, kinana apewa karipio

Kushoto ni Benard Membe,katikati Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana (kulia)
Na Tumaini Msowoya na Fortune Francis, Mwananchi 
Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania imemvua uanachama Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.
Wakati Membe akivuliwa uanachama, katibu mkuu wa zamani wa chama hicho
tawala, Abdulrahman Kinana amepewa karipio na kutakiwa kutogombea nafasi
yoyote ndani ya chama hicho kwa miezi 18 huku katibu mkuu mwingine wa
zamani Yusuf Makamba akisamehewa.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Februari 28, 2020 na katibu wa itikadi na
uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es
Salaam.
Polepole alikuwa akieleza uamuzi wa kamati kuu ambayo ilitoa siku saba
kwa kamati ya nidhamu iliyowahoji vigogo hao kukamilisha suala lao na
kuwasilisha taarifa.
Kinana, Makamba pamoja na Membe walihojiwa kwa nyakati tofauti Dodoma na
Dar es Salaam kutokana na kutuhumiwa kwa makosa ya kimaadili.
Agizo la viongozi hao kuhojiwa lilitolewa na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Mwanza, Desemba 13, 2019.
Wakati Membe akihojiwa Dodoma, Kinana na Makamba walikwenda katika ofisi
ndogo za Lumumba, mahojiano hayo yaliongozwa na Makamu mwenyekiti wa
CCM (Bara), Philip Mangula.
Vigogo hao walihojiwa baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya
kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto na jinsi chama
kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayejiita
mwanaharakati, ambaye alikuwa akitoa tuhuma dhidi yao.
Maamuzi kamati kuu
Polepole amesema kamati kuu imeazimia Membe afukuzwe uanachama, “uamuzi
huyu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonyesha
mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata
adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha lakini
imeonekana sivyo.”
“Adhabu ndani ya CCM kuna za siri ambazo ataambiwa mhusika na zinaweza
kuwa za wazi. Adhabu ya karipio na kufukuzwa zinasomwa hadharani.”
Amesema kamati kuu imepokea maelezo ya Kinana na imeazimia apewe adhabu
ya karipio kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za chama hicho
toleo la 2017.
“Adhabu ya karipio imeanishwa katika kanuni na inasema, ‘mwanachama
anayefanya kosa linalokipata matope chama na bila kuonyesha nia ya
kujirekebisha basi kamati kuu inaweza kumpa mwanachama huyo adhabu ya
karipio’.”
“Mwanachama aliyepewa adhabu ya karipio atakuwa katika hali ya matazamio
kwa muda usiopungua miezi 18 kutoka tarehe ya leo (Februari 28, 2020)
ili kumsaidia mwanachama huyu katika jitihada za kujirekebisha. Akiwa
katika kipindi hicho hatakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya
uongozi katika chama lakini atakuwa na haki ya kupiga kura kuchagua
viongozi wa chama kama ana dhamana hiyo.”
Kuhusu Makamba amesema, “baada ya fuatilia, kumhoji na kufuatilia
mwenendo wake, kamati kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Makamba
asamehewe makosa yake aliyotenda.”
“Imetoa msamaha huu kwa misingi kuwa Makamba wakati wote tangu
aliposomewa mashtaka yake amekuwa mtu muungwana, mnyenyekevu na mtii kwa
mamlaka ya chama. Kubwa kuliko yote ameomba msamehewe makosa yake kwa
barua zilizoambatanishwa katika maelezo yake. Amesamehewa makosa yake.”
SOMA ZAIDI <<HAPA>>
Via Mwananchi