Brela yajidhatiti utoaji wa huduma bora kwa wadau wake

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA akiwa katika
kikao cha kwanza na wafanyakazi tangu ateuliwe kilichofanyika katika
Ukumbi wa Mikutano BRELA Ofisi Kuu, Jijini Dar es Salaam.
**
Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni
(BRELA) imeweka mikakati mizuri katika kuhakikisha kwamba wadau wake
wanapata huduma yenye ubora.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa
katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano
BRELA Ofisi Kuu, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Bw. Nyaisa amewataka wafayakazi kufanya
kazi kwa bidii na kila mmoja kuwa tayari kusikiliza na kumsaidia mteja
punde anapokutana naye.
“BRELA ni Taasisi ya Umma na msingi wake ni kutoa huduma kwa Watanzania
wote katika hali ya haki na Usawa bila kujali tofauti za dini, kabila au
siasa”, alisema Bw. Nyaisa.
Akizungumzia kuhusu maoni ya wadau kuhusu changamoto ya mfumo, Bw.
Nyaisa amebainisha kwamba tayari suala la mfumo linafanyiwa kazi na
punde suala hilo litabaki kuwa historia.
“Changamoto ya mfumo wa usajili imezungumzwa na wadau wengi, hivi sasa
mfumo wa usajili unafanyiwa maboresho makubwa ili kurahisisha
upatikanaji wa huduma za BRELA kwa njia ya mtandao.
Sambamba na hilo uelewa kwa wadau wengi juu ya matumizi ya mfumo huu
bado upo chini, hivyo jitihada za ziada zimefanyika kuandaa kituo cha
miito ya simu mahususi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wadau wetu kwa
ukaribu zaidi”.Alibainisha Bw. Nyaisa.
Aidha Bw. Nyaisa ametoa wito kwa wadau BRELA kuendelea kuhuisha taarifa
za Makampuni na Majina ya Biashara yaliyosajiliwa nje ya mfumo wa
mtandao wakati changamoto wanazokutana nazo zikiendelea kufanyiwa kazi.

Wafanyakazi wa BRELA wakifuatilia kwa umakini maelekezo ya Afisa
Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa (hayupo pichani) katika kikao cha
wafanyakazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano BRELA Ofisi Kuu,
Jijini Dar es Salaam.