Chadema mkoa wa shinyanga wahamasisha wananchi kushiriki vema uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025

  

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi Town leo Ijumaa Juni 14,2024.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la makazi pamoja na daftari la kuduma la wapiga kura ili kushiriki vema katika uchaguzi wa serikali za mitaa Mwaka huu 2024 pamoja na uchaguzi mkuu Mwaka 2025.

Mhe. Ntobi ametoa wito huo leo Ijumaa Juni 14,2024 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ambao umeratibiwa na CHADEMA jimbo la Shinyanga mjini na kwamba umefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Town.

Amesisitiza wananchi wote kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ikiwa ni pamoja na kujiandikisha mapema katika daftari la makazi na kwamba hatua hiyo itasaidia kuchagua viongozi bora wanaowataka.

“Wananchi wa Shinyanga ili mpate viongozi sahihi wenye kupigania maslahi yenu, lazima mjitokeze kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi, na mjiandikishe mapema kwenye daftari la Makazi na daftari la kudumu la mpiga kura, ili mpate fursa ya kuchagua viongozi mnaowataka na siyo wakuchaguliwa ,”amesema Ntobi.

“Nampige kura kwa kuchagua Mtu na siyo Chama na kuna Uongo ambao unazushwa kwamba mkichagua wapinzani hamuwezi kupata Maendeleo, niwapeni tu mfano mimi nilipokuwa Diwani wa Ngokolo mbona nilipata Lami na sasa Ngokolo ina Lami, na zile Kata za CCM hakuna Lami, ikiwamo Kata ya Kambarage,”ameongeza Ntobi.

Pamoja na mambo mengine  Mhe. Ntobi ametumia nafasi hiyo kuitaka serikali kuongeza ubunifu kwenye vyanzo vya mapato ili kujiepusha na mikopo ambayo inaweza kurudisha nyuma maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini Bwana Hamisi Ngunila amesema Chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinasimamisha wagombea imara wenye kupigania maslahi ya wananchi katika kila nafasi ya uongozi.

Naye ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa jimbo la Shinyanga kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika kupigania haki ya kila  mmoja na maendeleo ya taifa.

Misalaba Media imezungumza na baadhi ya wananchi ambao wamehudhuria mkutano huo wameshukuru kwa elimu hiyo huku wakiahidi kuchagua viongozi bora.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi Town leo Ijumaa Juni 14,2024.

Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini Bwana Hamisi Ngunila akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi Town.


Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini Bwana Hamisi Ngunila akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi Town.