Dkt nchimbi.: kilimo cha korosho singida kuitangaza tanzania

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa akiangalia  mkorosho uliopandwa katika shamba
la pamoja la koshoro la Masigati  Wilayani Manyoni alipotembelea shamba
hilo hivi karibuni

Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye koti jeusi)  akitoa
maelezo ya shamba la pamoja la  Korosho  la Masigati Manyoni  kwa kundi
la wanachuo na wakufunzi  wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa waliotembelea
shamba hilo. Mwenye shati la kitenge ni Luteni Kanali RG Magemeson,
Mshauri wa Jeshi la Akiba  Mkoa wa Singida, anayefuata ni Mkufunzi,
Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Brigadia
Generali Liv Jian Mkufunzi wa chuo hicho

Picha
ya pamoja  baina ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi mwenye
kilemba na kikosi cha wakufunzi na wanachuo cha Ulinzi cha Taifa
walipotembelea shamba  la kilimo cha pamoja cha korosho wilayani Manyoni
hivi karibuni

Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye koti jeusi)  akiwa
pamoja  kundi la wanachuo na wakufunzi  wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa 
wakikagua shamba la kilimo cha pamoja la  Korosho eneo  la Masigati
Manyoni

Mshauri wa Jeshi la Akiba  Mkoa wa Singida,Luteni Kanali RG Magemeson (mwenye shati la kitenge), akipokea  zawadi ya  kiwekeo cha funguo kutoka kwa Mkuu wa msafara na  Mkufunzi
wa chuo hicho, Mhe. Balozi Peter Kallaghe baada ya kufanya kazi nzuri
ya kuratibu ziara hiyo wakiwa kwenye Mkoa wa Singida.
 

Na John Mapepele

Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amesema  uanzishaji wa mpango
wa kilimo cha pamoja (block farming) kwenye zaidi ya ekari 12000 wa zao
la korosho eneo la Masigati mkoani Singida umefanya eneo hili kuwa
miongoni mwa kivutio kikubwa cha utalii wa kilimo duniani utakaochangia
katika uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza
wakati wa kuwaaga wanachuo wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa waliotembelea
mradi wa shamba la kilimo cha pamoja cha Korosho Masigati wilayani
Manyoni leo, Dkt Nchimbi alisema Mkoa wa Singida unaendelea kufanya
mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kupitia mkakati wa kuwainua
wananchi wote baada ya kubuni kilimo cha pamoja ambapo alisema lengo ni
kila mwananchi apate angalau ekari kuanzia tano.

“Katika
kipindi hiki cha takribani miaka miwili tunashukuru Mungu kuwa tumeleta
mabadiliko makubwa ya kitabia na kifikra kwa wananchi wetu kupitia
mradi huu ambao wengi wao wameendelea kujiunga siku hadi siku na
kufurahia utajiri ardhi yao” alisitiza Dkt Nchimbi

Alisema
licha ya kupata ekari 12000 katika wilaya ya manyoni  pia wamepata
ekari 500 katika eneo la Itigi  na Ekari 500  kwenye eneo la Ikungi
ambazo zote zinaendelezwa kwa mtindo wa kilimo cha pamoja.

Dkt.
Nchimbi aliongeza kuwa mpango wa baadaye ni kuongeza eneo na kuanzisha
ushirika wa pamoja wa wakulima wa Korosho ambapo  pia wametenga maeneo
kwa ajili ya kujenga viwanda na maghara kwa ajili ya kuchakata na
kuhifadhia Korosho.

“Mpango
wetu wa baadaye kwenye eneo hili ni kuweka miundombinu ya kisasa na
viwanda vikubwa.Tunataka minada yote ifanyike hapahapa”alisisitiza Mkuu
wa Mkoa

Aidha
alitoa rai kwa wananchi popote nchini kuja kulima zao hilo kwenye  eneo
hilo huku akionya kuwa Serikali itamtoa mtu yoyote atakayebainika
kutumia eneo hilo kwa lengo lisilokusudiwa.

“Tunaelewa
wanakuja ili kupata hati ya eneo hili ili wafanye matumizi
mengine.Nawatangazia kuwa wasijidanganye kwa kuwa  hati inayotolewa
hapa  ni maalum kwa ajili ya kulima  zao la Korosho na siyo vinginevyo
hivyo tupo makini sana katika hilo” alisema

Alisema
kutokana na tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Kilimo ya Naliandele,
imeonyesha kuwa  eneo hilo ni bora ukilinganisha na maeneo mengi hapa
nchini na kwa kuwa  korosho za eneo hili zinawahi zaidi kukua na pia
zinazaa mara mbili kwa mwaka kutokana na eneo hili kuwa na misimu miwili
ya kiangaza hivyo kutoa maua mara mbili kwa mwaka mmoja.

Aidha
alisema  kutokana na eneo hili kuwa na umuhimu wa pekee katika kilimo
cha Korosho tayari taasisi mbalimbali za kilimo za Serikali zimeanzisha 
ofisi za kudumu ili kuwasaidia wananchi kwenye kilimo cha zao hilo.
Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Taasisi ya Utafiti wa kilimo
Naliandele na Bodi ya Korosho nchini.

Dkt.
Nchimbi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa John Pombe
Magufuli kwa  kutoa pikipiki nne kwa ajili ya kusadia kazi hiyo na
kwamba aliahidi jumla ya pikipiki kumi.

“Kipekee
kabisa nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu kwa  kweli yupo pamoja
na sisi katika  mpango huu ametutia nguvu sana, tunamwombea kwa Mwenyezi
Mungu  aishi miaka  mingi” alisema

Alisema
mapindunzi ya kijani ya kilimo cha Korosho yameifanya Singida  kuwa
tofauti na ya awali iliyosadikiwa kuwa Singida ya njaa,masikini, kame na
isiyokuwa na fursa ambapo hata watumishi wa umma walikuwa anakataa
kuhamia.

Alisema 
baada  ya kufanikiwa katika mradi huu mkoa unatarajia kuanzisha  mradi
mwingine kama huo kwa mazao ya kudumu baada ya kufanya tafiti za kutosha
ili kuinua uchumi wa wananchi wa kawaida wa mkoa huo.

Alisema
mkakati wa sasa ni kuufanya Singida kuwa mkoa wenye uchumi mkubwa kwa
kuwa mbali ya kuwa na rutuba na hali ya hewa nzuri pia una utajiri wa
raslimali za kutosha ikiwa ni pamoja na vivutio mbalimbali  vya
kihistoria kama kijiji cha kilimatinde ambacho kinahistoria ya kuwa
kituo cha njia kuu ya watumwa   toka miaka ya 1885 na ngome ya utawala
wa Mjerumani na Mwingireza, mabwawa makubwa ya samaki na kituo kikubwa 
duniani cha Hija kilichopo Sukamahela.

Kiongozi
wa msafara wa  Chuo Ulinzi cha Taifa, Mhe. Balozi Peter Kallaghe
alipongeza juhudi na mapinduzi makubwa yanayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa
Singida ambapo alisema  mageuzi haya yanapaswa kuigwa na  mikoa yote
hapa nchini ili kuunga mkono jitihada za kuifanya Tanzania kuwa Serikali
ya viwanda ifikapo 2025 yanayoongozwa na Rais John Pombe Joseph
Magufuli.