Eac yapoteza dola zaidi ya bilioni 37 katika sekta ya biashara kutokana na janga la covid-19

Ofisa Mkuu wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki Bwana Peter Mathuki

Na Mwandishi Wetu

Ofisa
Mkuu wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki Bwana Peter Mathuki
amesema, tangu janga la virusi vya Corona lilipotokea, nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepoteza zaidi ya dola bilioni 37, kutokana na
kukwama kwa shughuli nyingi za kibiashara .

Akizungumza na waandishi wa habari hivi
karibuni, Bw. Mathuki amezitaka nchi sita zinazounda Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), kushirikiana ili kutatua mizozo ya mipakani inayoathiri
biashara katika ukanda huo.

Katika
siku za hivi karibuni, madereva wa malori ya mizigo wanaotoka Kenya kwenda
Uganda, na wanaotoka Tanzania kuingia Kenya wamekuwa wakilalamika vikali
kuhusiana na masharti makali yaliyopo mipakani, yanayowalazimisha kukaa mpakani
kwa zaidi ya wiki moja, hali inayoathiri bidhaa nyingi haswa vyakula, kando na
kulemaza shughuli za kibiashara katika mataifa husika.

Bwana Peter Mathuki amesema, tayari Baraza
hilo limewaarifu mawaziri husika kutoka nchi sita wanachama wa Jumuiya hiyo,
ili kutafuta suluhisho la tatizo hilo.

Aidha,
Bw. Mathuki amesema, sekta ya utalii katika kanda ya Afrika Mashariki
imeathirika zaidi na kuchangia asilimia 92 ya hasara ya kibiashara katika kanda
hiyo.

Jumuiya
ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi,
Rwanda na Sudani ya Kusini.