Ewura yatoa msaada wa mashuka 431 kwa vituo vinne vya afya

 

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Godfrey
Chibulunje,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa msaada wa
mashuka 431 katika vituo vinne vya afya vilivyopo Jiji la Dodoma hafla
iliyofanyika leo June 23,2021 jijini Dodoma na kuhudhuruliwa na Mganga
Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dk. Andrew Method.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Godfrey
Chibulunje,(kulia) akimkabidhi sehemu ya mashuka Mganga Mkuu wa Jiji la
Dodoma, Dk. Andrew Method baada ya EWURA kutoa msaada wa mashuka 431
katika vituo vinne vya afya vilivyopo Jiji la Dodoma hafla iliyofanyika
leo June 23,2021 jijini Dodoma.

Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma,Dk.
Andrew Method ,akitoa neno la shukrani kwa EWURA baada ya kupokea
msaada wa mashuka 431 katika vituo vinne vya afya vilivyopo Jiji la
Dodoma iliyotolewa na EWURA hafla iliyofanyika leo June 23,2021 jijini
Dodoma.

Muonekano wa maboksi yakiwa na mashuka yalitolewa na EWURA

………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti
wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), imetoa msaada wa mashuka 431 kwa
vituo vinne vya afya vilivyopo Jiji la Dodoma yenye thamani ya
Sh.Milioni tano,ili kusaidia uboreshaji wa huduma za afya katika jiji
hilo ambalo linakabiliwa na ongezeko la idadi ya watu.

Akitoa msaada huo leo June 23,2021
jijini Dodoma ,Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Godfrey
Chibulunje,amesema kuwa wametoa msaada huo ili kuongeza kasi ya utoaji
huduma za afya kwa wananchi kupitia vituo vya afya vinne ambavyo ni
Makole, Mkonze, Hombolo na Kikombo.

Mhandisi Chibulunje
amesema kuwa msaada huo wameutoa ikiwa ni mchango wa EWURA kwa jamii
hususan katika kipindi hiki cha kuhitimisha wiki ya utumishi wa umma
nchini.

Amesema kuwa msaada huo utasambazwa katika vituo vya afya vilivyolengwa kwa kuzingatia mahitaji halisi katika kila kituo.

“Tumetoa msaada wa mashuka 431 kwa
Jiji la Dodoma na yataenda kwa vituo vinne cha Makole, Hombolo, Mkonze
na Kikombo, tumechangua mwaka huu eneo la afya ili kusaidia mwaka
mwingine tutachagua eneo jingine,”amesema Mhandisi Chibulunje

Mhandisi Chibulunje
amesema katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma, mamlaka hiyo imetoa
mafunzo kwa watumishi wake na kutembelea watoa huduma mbalimbali
wanaowasimamia kubaini changamoto wanazokabiliana nazo ili waweze
kuzitatua

”Lengo letu ni kuhakikisha mlaji anapata huduma bora kwa viwango vinavyosimamiwa na mamlaka yetu”ameeleza

Kwa upande wake,
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dk. Andrew Method,amesema kuwa Jiji hilo
linashukuru kwa msaada huo kwa kurejesha katika jamii kwenye sekta ya
afya.

Dk.Method amesema
kuwa kwa wastani katika Kituo cha Afya Makole, wajawazito 120
wanajifungua kila wiki, hivyo kwa mwezi idadi ya wajawazito
wanaojifungua katika kituo hicho inafikia 400 hadi 600.

”Tutahakikisha
msaada huo unatumika katika maeneo yaliyokusudiwa huku akiishukuru EWURA
kwa kuendelea kusaidia sekta ya afya kwa jiji hilo ambapo tayari
ilikwishatoa msaada wa vifaa vya kutunza watoto njiti.”amesema
Dk.Method