Ajali ya gari yaua wafanya biashara arusha

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, ACP Jonathan Shanna

 
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Jeshi la Polisi mkoani Arusha
linamshikilia dereva wa gari ndogo aina ya Toyota Salon yenye namba za
usajili T.213, Deogratius Thomas Kiwale, aliyesababisha vifo vya watu
watatu na kujeruhi wawili baada ya gari lake kuacha njia na kugonga
wafanyabiashara na watembea kwa miguu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 9,
2019 na Kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Jonathan Shanna, ambapo
amesema kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 1:00
usiku, katika barabara ya Arusha Moshi maeneo ya Manchester, Kata ya
Sekei Halmashauri ya Jiji la Arusha.

“Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa
dereva kushindwa kulimudu gari lake hali iliyopelekea vifo na majeruhi,
Dereva wa gari hilo amekamatwa na pindi upelelezi utakapokamilika
atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria” amesema ACP Shanna.

ACP Shanna ameyataja majina ya watu
waliofariki na kupatwa na majeraha katika ajali hiyo kuwa ni Gudla
Mashanga, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari, Honorina Zakaria,
mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari, Amina Hassan mkazi wa Moivo, ambapo
majeruhi ni Rogath Minja, mfanyabiashara na mkazi wa Sanawari na
Renatha Thadei ambaye pia ni mfanyabiashara na mkazi wa Sekei.

Kwa mujibu wa Kamanda Shanna, miili ya
marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru, na majeruhi pia
wamelazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi.