Joyce Joliga Namtumbo
Taasisi ya Moyo JKCI inatarajia kuitumia Hospitali ya Wilaya Namtumbo kama kituo kidogo cha uchunguzi na Matibabu ya moyo ili kusaidia wananchi wenye hali ya chini mkoani Ruvuma na mikoa jirani kupata matibabu karibu na maeneo wanayoishi na kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kwenda kufuata matibabu.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa jimbo la Namtumbo Vita Kawawa wakati wa uzinduzi wa kambi ya maalumu ya uchunguzi na matiabu ya moyo ambayo inaendeshwa na Madaktari bingwa tisa wa moyo toka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambayo imeanza rasmi leo 10 hadi 13 Julai 2024.
Kawawa amesema Mkurugenzi wa Taasisi ya JKCI Dkt.Peter Kisenge ameahidi kupeleka vifaa na wataalam ili kusaidia kutibu wananchi wenye matatizo ya moyo pamoja na kuwapatia watumishi mafunzo ya awali ya kutumia vifaa ili kutoa tiba ya awali ya utambuzi wa ugonjwa wa moyo.
Amesema,kupelekwa kwa huduma ya matibabu ya moyo wilayani humo kutasaidia kupunguza kero ya wananchi kusafiri umbali mrefu kwenda kufata huduma ya matibabu Hospitali ya Rufaa Muhimbili , Bugando na KCMC.
“Namshukuru sana mkuu wa JKCI kwa kutupatia wataalam hawa, pia ameahidi kutuletea vifaa na kututafutia wafadhili na ametangaza kwanzia sasa Hospitali ya Namtumbo itakuwa kituo kidogo cha JKCI ili wananchi waweze kupatiwa matibabu hapahapa na madaktari bingwa toka JKCI;”Alisema Kawawa.
Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuleta huduma ya mkoba katika wilaya hiyo kwani itatusaidia wananchi na pia ameweza kupeleka vifaa tiba, Dawa na hata kuboresha miundombinu ya majengo
Naye Kiongozi wa Madaktari bingwa tisa wa moyo Dr.Baraka Ndelwa toka taasisi ya Moyo JKCI amesema , Wagonjwa wote watakaojitokeza watapatiwa matibabu hata kama ni usiku .
” Tunauzoefu wa wa kuhudumia wagonjwa wasiopungua 400 na watahakikisha wanawahudumia wagonjwa wote ambao watajitokeza.”Alisema Dkt Ndelwa.
Dr.Aaron Hyera ,amesema wataalam watawasaidia wananchi wenye uwezo mdogo kupata uchunguzi wa afya zao na matibabu wakiwa kwenye maeneo yao
“Hii ni mara ya tatu kwa madaktari bingwa kuweka kambi wilayani hapo hivyo amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuweza kupata matibabu.”,alisema Dkt Hyera
Naye Theodora Mhuwa mkazi wa kijiji cha Likuyuseka amesema ameteseka kwa muda mrefu na ugonjwa wa moyo kutokana na kutokuwa kuwa na uwezo wa kupata fedha za matibabu hivyo alishakata tamaa na kusubiri kifo hivyo kupelekwa kwa huduma hiyo kutasaidia wananchi kupata huduma za moyo toka kwa madaktari bingwa.
Kwa upande wake Halima Shauri mkazi wa kijiji cha Njalamatata amesema amepitia mateso makubwa ya kusafiri mara kwa mara kwenda Muhimbili kutibiwa tatizo la moyo hivyo kupelekwa kwa huduma hiyo kumerejesha matumaini mapya kwa wagonjwa wa moyo.
“Niwaombe wananchi wajitoleze kufanyiwa uchunguzi na kutibiwa ili waweze kufahamu matatizo yanayowakabili “