Jumla ya miradi 151 inatarajiwa kuwekeza mtaji wa dola milioni 987.04 katika kipindi cha mwezi julai 2020-machi 2021

 

Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi
akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za kituo hicho
Jijini Dar es Salaam. Baadhi
ya watumishi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakifuatilia mkutano
wa waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za kituo hicho leo
Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi akipata
picha ya pamoja na waandishi wa habari katika ofisi za kituo hicho leo
Jijini Dar es Salaam.

PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO

NA EMMANUEL MBATILO

Katika kipindi cha mwezi Julai 2020
hadi Machi 2021, Jumla ya miradi 151 imesajiliwa ambayo inatarajiwa
kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 987.04 na kutoa ajira 13,857.

Ameyasema hayo leo Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kituo hicho Jijini
Dar es Salaam.

Dkt.Kazi amesema ikilinganishwa na
kipindi kama hiki mwaka jana ambapo kituo kilisajili miradi 169, idadi
ya miradi imepungua kunatokana na athari za janga la ugonjwa wa korona
Duniani.

“Sekta ya viwanda imeendelea kuongoza
katika miradi iliyosajiliwa katika kituo cha Uwekezaji Tanzania ambapo
imesajili jumla ya miradi 94 (62.25%) yenye mtaji wa jumla ya Dola za
Marekani milioni 463.17 (46.9%), na inakadiriwa kutoa ajira kwa
watanzania wapatao 9,220”. Amesema Dkt.Kazi.

Aidha Dkt.Kazi amesema Katika kipindi
cha mwezi Januari hadi Machi, 2021 kituo cha Uwekezaji kimefanikiwa
kusajili jumla ya miradi mipya 51 ambapo mtaji unaotarajiwa kuwekezwa wa
Dola za Marekani milioni 451 umeongezeka kwa asilimia 63 na ajira mpya
4,272 zinazotarajiwa kuzalishwa zimeongezeka kwa asilimia 3.5
kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana ambapo kituo kilisajili
miradi 54.

Pamoja na hayo Dkt.Kazi amesema katika
siku za hivi karibuni wawekezaji wengi na mabalozi na wawekilishi wa
mashirika ya kimataifa wameonyesha kufurahishwa na mwenendo wa serikali
katika suala zima la kuboresha mazingira ya uwekezaji na tayari wameanza
kuonyesha nia ya kusaidia programu mbalombali za maboresho ya mazingira
ya uwekezaji nchini.