Kabudi: hakuna mwenye uwezo wa kubadili ukomo wa rais wa awamu mbili


Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba
Kabudi amesema hakuna mtu yoyote mwenye uwezo wa kubadili ukomo wa urais
wa awamu mbili huku akisisitiza hilo haliwezekani katu.


Profesa
Kabudi amesema hayo jana wakati akifungua kongamano la Kumbukizi ya
Mwalimu Julius Nyerere ambapo mada kuu ilikuwa inasema miaka 20 baada ya
Mwalimu.Profesa Kabudi alikuwa amemuwakilisha Rais Dk.John Magufuli
ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Wakati
anatoa hotuba yake Profesa Kabudi alisema kuwa hakuna wa kubadili awamu
mbili za uongozi wa urais.”Tutaendelea na vipindi viwili vya ukomo wa
urais, na kesi iliyofungulia na moja ya raia wa Tanzania kuhusu ukomo wa
Rais, isihusishwe na Rais wa sasa.”

Alifafanua
kwamba vipindi vya urais ni sehemu ya tunu iliyoachwa na Mwalimu
Nyerere na hivyo kila mmoja wetu analojukumu la kuilinda tunu hiyo
ambayo imeweka utaratibu mzuri kuhusu ukomo wa Rais.

Profesa
Kabudi ametumia nafasi hiyo kuelezea pia uamuzi wa Mwalimu Nyerere
katika mfumo wa vyama vingi ambao aliuruhu lakini katika mfumo wa
kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na umoja, amani na mshikamano.

Ambapo
katika eneo hilo la vyama vingi mbali ya kuwa sehemu ya kumuenzi
Mwalimu Nyerere, ametumia kuhimiza Watanzania wa kada mbalimbali kusoma
sheria mpya ya vyama vya siasa ambayo kwa sehemu kubwa imefanyiwa
marekebisho.

“Moja
ya marekebisho ndani ya sheria ya vyama vingi, inazungumzia umuhimu wa
vyama vya siasa kufanya uchaguzi za ndani kwa ajili ya kubadilishana
uongozi na wanawake kushirikishwa.

“Pia
katika sheria hiyo imezungumza kwa kina suala la uwazi kuhusu vyanzo
vya fedha pamoja na matumizi yake ambayo yanatakiwa kuwa wazi na
kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.Pia sheria
hiyo inapiga marufuku kuwa na vyama vya siasa vyenye muelekeo wa udini,
kuligawa taifa na fujo na kueneza chuki miongoni mwetu,”amesema Profesa
Kabudi.

Aliongeza
kuwa sheria hiyo pia inatoa maelekezo mafunzo na itikadi
zinazofundishwa ndani ya vyama vya siasa lazima Msajili wa Vyama vya
Siasa apewe taarifa na kushiriki kwenye mafunzo hayo.

Profesa
Kabudi wakati anazungumzia mambo ya kumuenzi Mwalimu Nyerere amegusia
suala la utaifa na hasa katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili
inaunganisha wananchi wote bila kujali makabila zaidi ya 120 yaliyopo
nchini.

“Kuna
mambo mengi ambayo nchi yetu inaendelea kufanya kama sehemu ya kuenzi
misingi ambayo wengine wanaita tunu iliyoachwa na Mwalimu Nyerere.Hata
hivyo Rais wetu Dk.Magufuli kuna mambo mengi anafanya kwa ajili ya
kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Nyerere,”amesema Profesa Kabudi.

Alitaja
baadhi ya mambo ya hayo ni utekelezwaji wa miradi mikubwa nchini ambayo
inafahamika kama miradi ya kimkakati ukiwemo uamuzi wa Serikali ya
Awamu ya Tano kuhamia rasmi Dodoma kwani huo ulikuwa mpango wa Mwalimu
lakini hakufanikiwa kuutekeleza.Pia ujenzi wa mradi wa umeme katika
bwawa la Mto Rufiji ambalo kwa sasa linafahamika kama Mwalimu Nyerere
Hydro Power Project utakaozalisha megawati 2115 na utagharimu zaidi ya
Sh.trilioni 7 fedha ambazo ni za ndani.

Pamoja
na hayo Profesa Kabudi amezungumzia ujenzi wa reli ya kisasa ambayo
awamu ya kwanza ya ujenzi imeanza Dar es Salaam hadi Dodoma.”Mwalimu
Nyerere aliwapenda sana Watanzania na hivyo alikuwa na ndoto ya kuona
wanakuwa na uchumi wa kati , hivyo Rais Magufuli ameibeba ajenda hiyo
kwa vitendo ambapo ndani ya miaka minne ya uongozi wake amehakikisha
amejenga na anaendelea kujenga miradi mbalimbali ya kimandeleo.

“Na
katika hilo Serikali imeamua kwa vitendo kuboresha huduma za afya kwa
kujenga vituo 352 na kwa ujenzi wa kila kituo umegharimu Sh.milioni 500
tofauti na hapo awali ambapo gharama za ujenzi zilikuwa kubwa sana na
mkapaka sasa kuna maombi ya ujenzi wa viwanda nane vya dawa
nchini,”amesema.

Ameongeza
kuwa katika kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye alihakikisha watu wake
wanapata elimu, Rais Magufuli ameamua kutoa elimu bure huku akifafanua
kuwa kama Watanzania wanakumbuka Rais baada ya kuapishwa alikaa miezi
mitatu bila ya kuwa na baraza la mawaziri ili fedha za kuwalipa zitumike
kusomesha watoto.

“Uamuzi
wa Rais kutoa elimu bure, umeongeza idadi ya uandikishwaji wa wanafunzi
kwa asilimia 20.1 .Hali hiyo imeongeza pia idadi ya watoto wanaojiunga
na masomo ya sekondari,”amesema Profesa Kabudi.

Katika
eneo la maji Profesa Kabudi amesema kuwa ni moja ya changamoto kubwa
lakini Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wake
wanapata maji safi na salama.

“Nilikuwa
kwenye ziara ya Rais, tukiwa huki tumekutana na changamoto ya uhaba wa
maji.Nakumbuka siku za karibuni nilikuwa Marekani ambako huko nilikuwa
nalala kwenye hoteli ya hadhi ya nyota tano lakini baada ya kurudi na
kuungana na Rais kwenye ziara nimelala gesti ya kawaida ambayo maji ya
kuoga tunateka kwa ndoo,”amesema.

Kuhusu
mikataba Profesa Kabudi amesema kuwa iliyopo sio kwamba haikuwa halali
lakini Rais Magufuli kwa mapenzi mema aliyonayo kwa wananchi wake ameona
ni vema ikapitiwa ili kuleta tija kwa watu wote tofauti na awali.

“Ndio
maana Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kupitia upya mikataba ya madini
na leo hii wote tunaona faida yake.Pia mkataba wa Kampuni ya simu ya
Airtel ambao umepitiwa upya na sasa tunanufaika na uwepo wa kampuni
hiyo.Niwaambie tu pamoja na Serikali kuwa na hisa bado kila mwezi
tunapata Sh.bilioni moja kutoka kampuni hiyo na itakuwa hivyo kwa
kipindi cha miezi 60,”amesema Profesa Kabudi.

Hata
hivyo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuenzi mambo ya msingi ambayo
yameachwa na Mwalimu Nyerere kwa maslahi ya Taifa letu la Tanzania.