Kamanda magomi atoa taarifa ya misako na doria, mali na vielelezo mbalimbali vya wizi vyakamatwa mkoani shinyanga


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga katika
kuendelea kuimarisha  ulinzi na usalama
wa raia na mali zao kwa  kipindi cha
mwezi mmoja limefanya doria na misako mbalimbali ambapo limefanikiwa kukamata
mali na vielelezo mbalimbali vya wizi.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa
habari leo Oktoba 12,2023, kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga
kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi ameeleza kuwa jeshi hilo kwa kipindi
cha mwezi Septemba 2023, watuhumiwa 25 wameshikilia kwa makosa mbalimbali
ikiwemo uuzaji wa madawa ya binadamu kiholela katika maduka binafsi ya dawa.

Amesema jeshi hilo limewafikisha
mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali na kuhukumiwa ikiwemo kesi za
kubaka, kesi ya kulawiti, pamoja na kesi mbili za wizi wa mtoto.

“Kwa
kipindi cha mwezi mmoja uliopita tumefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa
wa kesi mbalimbali na kuhukumiwa kama ifuatavyo kesi tano za kubaka
zilihukumiwa kifungo cha miata 30 jela, kesi moja ya kulawiti ilihukumiwa
kifungo cha miaka 30 jela na nyingine kama hiyo ilihukumiwa kifungo cha  maisha jela pia kesi mbali za wizi wa mtoto
zilihukumiwa kifungo kati ya miaka mitano na mitatu jela, kesi moja ya
kujiwasilisha ilihukumiwa kufungo cha miezi 13 jela huku kesi moja ya wizi wa
mifugo ikihukumiwa kutumikia jamii kwa mwaka mmoja, makosa sita ya wizi
yalihukumiwa kifungo kati ya miaka mitano hadi miezi sita jela”.amesema Kamanda
Magomi

“Tulifanya
misako na doria katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga na kufanikiwa
kukamata mali na vielelezo mbalimbali kama ifuatavyo tumekamata madawa
mbalimbali ya binadamu ambayo yalikuwa yanauzwa kuholela katika maduka binafsi
ya madawa na pia vifaa tiba mbalimbali katika msako wa pamoja na TMDA, afya na
afisa biashara uliojulikana kama operesheni pangea kama ifuatavyo. Boksi moja la
sindano, boksi moja la mipira drip, boksi moja la chupa za maji ya drip boksi
moja la dawa mchanganyiko pia tumekamata boksi tatu za  vipodozi vyenye viambata vya sumu na boksi
moja la taulo za kike”.amesema Kamanda Magomi

“Vilevile
tumekamata viroba vitano vya mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku nchini
thamani ya mifuko hiyo bado haijafahamika lakini pia tumekamata mirungi bunda
20, bangi gramu 1800, lita tano za pombe haramu ya moshi, vitu mbalimbali
vilivyokuwa vikitumika kupiga ramli chonganishi pamoja na pikipiki sita ambazo
zilikuwa zinatumika katika uhalifu sehemu mbalimbali”.

“Jumla
ya watuhumiwa 25 wanashikiliwa katika vituo mbalimbali vya Polisi kwa tuhuma
hizo huku wengine wakiwa wameshafikishwa mahakamani na kupewa dhamana”.amesema
Kamanda Magomi

Aidha kamanda Magomi amesema katika kipindi
hicho jeshi la Polisi lilifanya operesheni za usalama barabarani na kukamata
jumla ya makosa 3080 yakiwemo makosa ya magari 2331 na kwamba upande wa
pikipiki na bajaji zilikamatwa  749.

Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa
wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kufuata sheria za usalama barabarani naza nchi
kwa ujumla hususan katika kipindi hiki cha mwisho wa Mwaka ili kulinda amani na
utulivu uliopo.

  

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi akionesha vitu mbalimbali vilivyokamatwa na jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi Septemba 2023.