Kamati ya bunge yaipongeza ofisi ya waziri mkuu kwa mkakati wa ajira na uwezeshaji vikundi vya vijana

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga akizungumza na wajumbe wa
kamati hiyo pamoja na watendaji wa halmashauri ya Morogoro
walipotembelea Mkoa huo kwa lengo la kukagua miradi ya vijana
walionufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mikopo kupitia mapato ya
ndani ya halmashauri.




Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akielezea
jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria walipofanya
ziara ya kukagua miradi ya vijana Mkoani Morogoro. Kulia ni Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga



Kiongozi wa Kikundi cha Vijana cha
Mazimbu Agro Enterprise Bw. Alexander Jokonia (wa nne kutoka kushoto)
akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria
walipowatembelea katika eneo lao la kazi kujionea miradi ya kiuchumi
inayofanywa na vijana katika Mkoa wa Morogoro. Kikundi hicho kimenufaika
na mkopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu.



Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga wakipitia taarifa ya mradi wa
vijana wa Mazimbu Agro Enterprise. (Katikati) ni Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde.



Kiongozi wa Kikundi cha Vijana cha
Faraja Carpentry Bw. James Luwanda akionyesha vitendea kazi
wanavyotumia kutengeneza bidhaa zao. Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde. (Wa pili kutoka
kushoto) ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria
Mhe. Najma Giga.



Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria wakipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha
Vijana cha Faraja Carpentry Bw. James Luwanda namna wanavyobuni urembo
(nakshi) katika meza ya chakula “Dinning Table”.



Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria wakiangalia kitanda kilichotengenezwa na Kikundi cha
Vijana cha Faraja Carpentry kilichopo Mkoani Morogoro. (Wa tano kutoka
kulia) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe.
Anthony Mavunde. (Wa nne kutoka kushoto) ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga.


PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU


(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)


………………………..


Na; Mwandishi Wetu


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu kwa mikakati iliyoweka katika kuwajengea uwezo vijana
kujiajiri na uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana “Youth Development Fund” na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya
halmashauri.


Akizungumza wakati wa ziara ya
ukaguzi wa miradi ya vijana katika Mkoa wa Morogoro, Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga ameipongeza
Serikali kwa mikakati iliyokuja nayo katika kutatua changamoto ya
ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na
yanayowahamasisha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.


“Matokeo ya utekelezaji wa
mikakati hiyo tumeona kwa kiasi kikubwa imewawezesha vijana kutambua
taratibu rasmi za kupata mikopo yenye riba nafuu na ambayo imewasaidia
kuazisha miradi ya kiuchumi,” alisema Mheshimiwa Giga.


Aliongeza kuwa Serikali iendelee
kutenga bajeti zaidi ya uwezeshwaji wa vikundi vya vijana kwa kuwa vina
tija na vinapunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.


Sambamba na hayo Kamati hiyo
iliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutoa maelekezo katika
halmashauri zote kuelimisha vijana zaidi ili waweze kutambua taratibu za
kupata mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na asilimia 10 ya
mikopo ambayo utolewa kwa Vijana 4%, Wanawake 4% na Wenye Ulemavu 2%
kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.


Akitoa maelezo ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi,
Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Bunge
kwamba Serikali itaendelea kuviwezesha kiuchumi vikundi vya vijana
katika mkakati wa kuhamasisha vijana kujiajiri lakini pia kuwajengea
uwezo wa kiuchumi vijana ili nao pia washiriki kikamilifu katika
mnyororo mzima wa uchumi wa viwanda ambapo matarajio ni kwamba ifikapo
mwaka 2025 zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi iwe imeajiriwa kwenye sekta
ya viwanda.


“Serikali iliazisha mfuko wa
maendeleo ya vijana na programu mbalimbali ili kuwawezesha wananchi
hususan vijana kuweza kupata mahitaji ya mitaji ya kuanzisha shughuli za
kiuchumi zitakazo waingizia kipato,” alisema Mavunde


Akitolea mfano mafunzo ya kilimo
cha kisasa kwa vijana kutumia teknolojia ya kitalu nyumba ni mkakati
mzuri ambao Serikali imekuja nao katika kutatua tatizo la ajira kwa
vijana kupitia sekta ya kilimo.


Aidha, Naibu Waziri Mavunde
aliwahamasisha vijana kuandaa maandiko ambayo yataelezea shughuli zenye
tija wanazotaka kuzifanya katika kujileta maendeleo ili waweze kupata
mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana na Mikopo kupitia mapato ya
ndani ya halmashauri itakayowasaidia kuendesha shughuli zao. 


Kwa nyakati tofauti vijana wa Mkoa
wa Morogoro wameishukuru Serikali kwa uwezeshaji kupitia Mfuko wa
maendeleo ya vijana na kuomba kuwezeshwa zaidi ili kukidhi matarajio yao
ya uanzishwaji wa viwanda katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Tano katika uchumi wa viwanda.