Kesi ya erick kabendera yapigwa kalenda hadi january 27

Upande
wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwandishi wa
habari za uchunguzi Erick Kabendera, umeielezea Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kuwa upelelezi katika kesi hiyo umebakia katika maeneo machache
kukamilika. 


Wakili
wa Serikali, Ester Martin ameileleza Mahakamani hiyo jana  Jumatatu,
Januari 13, 2020 wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Martin
alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Janeth Mtega
upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kwamba wanamalizia vitu
vichache ili kukamilisha upelelezi wa shauri hilo.

Hakimu Mtega baada ya kueleza hayo, aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 27, 2020 itakapotajwa.
Kabendera
anakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kutakatisha fedha kiasi cha
Sh173 milioni, katika Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam.