Kikwete akerwa na wanaotafsiri vibaya hotuba yake

Ofisi ya Rais mstaafu wa awamu ya Nne
Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, imewataka baadhi ya watu kuacha kutoa tafsiri
isiyo sahihi, kuhusu alichokizungumza katika kongamano la kumbukizi ya
miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere. 
Taarifa hiyo iliyotolewa usiku wa
kuamkia leo Oktoba 11, imeeleza masikitiko yake kuhusu upotoshaji
unaofanywa na baadhi ya watu, kuhusu hotuba aliyoitoa Oktoba 8, 2019,
katika Kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere Kivukoni.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika
kongamano hilo Rais Mstaafu, alieleza namna alivyokuwa akimfahamu Hayati
Baba wa Taifa, lakini kilichowashangaza ni kujitokeza kwa baadhi ya
watu wachache wanaopotosha ukweli kuhusu maneno aliyoyasema kwa kujaribu
kuweka maneno ambayo hakuyatamka kinywani mwake kwa madai ya kuwa
anawasema baadhi ya viongozi waliopo sasa.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, Dkt
Kikwete, hakufanya ulinganifu wowote kati ya Mwalimu Nyerere na marais
waliopo na waliomaliza muda wao na kwamba huo ni uzandiki, fitna na
uchonganishi.