Kura za maoni katika kijiji cha diguzi zazua mzozo,wakulima waja juu

NA MWAMVUA MWINYI

WANACHAMA wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kijiji cha Diguzi ,Kata ya Matuli Morogoro vijijini
mkoa wa Morogoro, wameuangukia uongozi wa CCM wilaya,mkoa na hata Taifa
kufuatili kura za maoni kijijini hapo, ambapo yupo mgombea aliyeshinda
katika kura hizo kisha kukatwa kwa hali isiyoeleweka.
 

Wakizungumza na
Waandishi wa Habari, baadhi ya wakazi Maulid Lwambo, Ramadhani Makwangu,
Amini Jonathani na Aisha Mohamed wamesikitishwa na hatua ya kukatwa
jina la Nassoro Ramadhani ambae alishinda kwenye mchakato huo.
 

“Diwani Luca Lumomo
anatusumbua sana, huyu ni jamii ya mfugaji, hivyo anataka kutumia nafasi
yake kutaka kukiteka kijiji chetu kukifanya kiwe cha wafugaji, kwa kuwa
yeye ni mfugaji hivyo anatumia nafasi hiyo kutaka Mwenyekiti wa kijiji
chetu nae awe mfugaji,” alisema Lwambo.
 

Ameuomba uongozi wa
juu wa CCM uangalie figisu hizo wanazofanyiwa huku wakidai diwani wao
amekuwa tatizo kubwa kwa maendeleo ya kiniji chao.
 

Nae Ramadhani
anayetetea kiti hicho alisema kuwa anafanyiwa figisu hizo  ili mmoja wa
wagombea anaetakiwa na baadhi ya viongozi apite.
 

Nae Lumomo alikanusha
kujihusisha na figisu zinazotajwa, huku akisema kuwa kulikuwa na
ongezeko la wana-CCM siku moja kabla ya kufanyika kwa kura za maoni,
hatua iliyomlazimu mgombea wao nafasi hiyo kupinga.
 

Katibu Mwenezi wa
chama hicho Mkoa wa Morogoro Anthony Mhando alieleza taarifa hizo
anazisikia lakini hazijamfikia rasmi katika ofisi yake.
 

Alisema yeyote mwenye
malalamiko afike ofisi za chama kukaa kiti kimoja kujua tatizo lilipo
ili kuimarisha chama na kuendelea na uchaguzi kwa amani.