Likizo ya korona yawakimbiza watoto mtaani

 Na Mwandishi Wetu, Arusha.

WIKI chache baada ya serikali kuzifunga shule pamoja vyuo vyote nchini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu yaani CORONA kumeibuka wimbi kubwa la watoto wadogo wanaofanya biashara ndogondogo katika masoko jijini hapa.

Watoto hao wamekuwa wakionekana katika masoko hayo wakifanya biashara ndogondogo kama vile kuuza mifuko, viungo vya vyakula pamoja na kubeba mizogo ya wateja wanaofika katika masoko hayo kwa ajili kufanya ununuzi wa mahitaji yao.

Wafanyabiasha na wakazi wa maeneo hayo wameitaka serikali kuingilia kati kwani kufungwa kwa shule hakumaanishi watoto wazurure hovyo au wafanye kazi katika mazingira hatarini kama sokoni bali wanapaswa kutumia muda huo kujisomea.

Wakizungumza na JAMHURI baadhi ya wafanyabiashara katika masoko hayo wamesema watoto wamekuwa wakizunguka kutoka soko moja hadi jingine kutokana na uwepo wa soko kwa siku husika kwani kuna masoko ya kudumu kwa maana ya kila siku na yale ya siku moja moja kama vile minada.

Hassan Issa mfanyabiashara katika soko kuu la jijini Arusha amesema idadi ya watoto hao imeongezeka baada ya serikali kufunga shule na kwamba watu wengi wamekuwa wakiwatumia watoto katika kubeba mizigo kwa sababu malipo yao ni kidogo ikilinganishwa na watu wazima.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Meru Restituta Mvungi amekiri kuwapo kwa watoto katika masoko yaliyopo wilayani humo likiwemo soko la Tengeru na kwamba alishafanya mazungumzo yasiyo rasmi na watoto hao ambapo walikiri kuwa wengi wao ni wanafunzi na kwamba wanatafuta hela za matumizi.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya wilaya Arusha Neema Mwina amekiri kuwa wengi wao wanatoka katika halmashauri yake na kwamba mwaka juzi walifanya zoezi la kuwaondoa kwa kutumia migambo lakini  baada ya muda wamerudi tena hivyo ni wazi kuwa wanatakiwa kubuni mbinu mpya.

“Katika zoezi ile watoto zaidi 30 tuliwakamata, wengi wao walitupeleka makwao ingawa tulipata changamoto ya baadhi yao kututoroka njiani kutokana na usafiri tulioutumia, na nikagundua kuwa familia zinachangia tatizo hilo kwani wengi wa wazazi hawafuatilii maendeleo ya mtoto shuleni” Alisema Mwina

Mwenyekiti wa wafanyabiashara soko la Kilombero Abdi Mchomvu amesema uongozi wa soko hilo kwa kushirikiana na ofisi ya kata ya Levolosi waliendesha operesheni ya kuwaondoa lakini baada ya muda watoto hao wakarudi tena sokoni
na kuendelea na biashara hiyo.