Mahiga awataka wakuu wa magereza nchini kutumia ujuzi wa wafungwa kujiendesha na kutoa mchango wa gawio kwa serikali

Waziri
wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Balozi Dkt Augustine Mahiga amewataka
Wakuu wa Magereza nchini kutumia nguvu kazi na ujuzi wa wafungwa walioko
magerezani kubuni miradi mbalimbal ili kuwazalishia fedha
zitakazowawezesha kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.


Balozi
Mahiga ameyasema hayo jana alipotembelea gereza la Kyela kujionea jinsi
Taasisi za Haki Jinai zinavyotekeleza majukumu yake katika mahakama na
magereza ikiwemo kutatua changamoto ya mrundikano wa mahabusu katika
magereza pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji haki na hali ya magereza
kote nchini.

“Nguvu
kazi za hawa wafungwa ni nyingi na wana ujuzi mbalimbali mnaoweza
kuutumia kuanzisha miradi ambayo itawasaidia kupata fedha na mkaweza
kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini, watumieni. Pale Dar
es Salaam natazama yale majengo ya magereza mnajengewa na jeshi wakati
mngeweza kujenga wenyewe.”

Kwa
upande wake Mkuu wa Gereza la Kyela ASP. Nelson.M. Mwaifani amesema
kwamba wao wamejitahidi kuhakikisha kwamba gereza hilo halina msongamano
wa mahabusu na kwamba mazingira ya wafungwa na mahabusu ni mazuri
salama kwa afya za watu hao kwani wana mabweni na magodoro yanayowatosha
wafungwa na mahabusu wote waliopo katika gereza hilo. Pamoja na hayo
ASP. Mwaifani amemwambia Waziri Mahiga aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu
wa Mashtaka Biswalo Mganga kwamba wameingia mkataba na Halmashauri ya
Wilaya ya Kyela ya kuzoa taka ngumu, kuzibua mifereji na kufanya usafi
katika hospitali ya Wilaya kwa makubalino ya kulipwa shilingi
6,700,000/- kwa mwezi.

Hata
hivyo, Dkt. Mahiga alifurahishwa na uongozi wa gereza la Kyela chini ya
ASP. Nelson.M. Mwaifani kwa kuwa wabunifu na kushirikiana vizuri na
Halmashauri ya Kyela kiasi cha kufanikiwa kupata tenda ya kufanya usafi
katika Halmashauri hiyo jambo linalowaingizia wastani wa cha shilingi
milioni sita kwa mwezi. Aidha aliwataka wakuu wote wa Magereza nchini
kuiga mfano huo na kwamba siku moja wawe sehemu ya taasisi za serikali
zitakazotoa gawio mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.
Dkt John Joseph Pombe Magufuli.

“Nataka
siku moja gereza hili lichangie kwenye mgao wa pesa za Taasisi ya
Mahakama kwaajili ya gawio la kwenda serikalini mbele ya Rais,
nikisikia, nitafurahi sana. Nina uhakika hivi karibuni tutaulizwa
mchango wenu ni nini kwenye gawio la serikali. Najua mnaweza kuwa vyanzo
vingi vya kupata pesa hivyo ni matumaini yangu kuwa gawio lijalo Wizara
yetu au Taasisi ndani ya wizara yetu itatoa kitu (‘very signficant’)
kikubwa, na magereza nina uhakika. Kule sabasaba kila mwaka mnapata
zawadi tena nzuri tu, mnaongoza, sasa hapa onesheni mfano mzuri.”
Amesema Dkt. Mahiga.

Hivi
Karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli azitaka
Taasisi za Umma zinazozalisha na kupata faida zitoe gawio kwa serikali
na kuzipa siku 60 Taasisi,Mashirika na Makampuni ya serikali ambayo
hajatoa yafanye hivyo ndani ya muda huo. Waziri Mahiga ameamua kutumia
ziara yake ya siku saba pamoja na mambo mengine kuzipa changamoto
Taasisi za utoaji haki jinai kuanza kufikiria namna ya kuweka mikakati
madhubuti ili nazo zianze kutoa gawio kwa serikali. Ziara hii
iliyoendelea leo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela na Gereza la
Kyela, itaendelea tena kesho katika Wilaya ya Mbarali jijini Mbeya.