Mameneja wa tanesco wakutana arusha kujadili tatizo la kukatika umeme mara kwa mara

Na Woinde Shizza, APC BLOG, ARUSHA

SHIRIKA la umeme Tanzania limesema kuwa  katizo la umeme la mara kwa mara
linaloendelea hivi sasa kikomo chake kitakuwa mwaka 2025 na wananchi watakuwa
wamesahau kabisa shida hiyo.


Hayo yamebainishwa na kaimu Naibu mkurugenzi Mtendaji wa
shirika la umeme Tanzania (Tanesco )Mhandisi Raymond Seya wakati akiongea na waandishi
wa habari mara baada ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo wahandisi wa
matengenezo na  Mameneja wa shirika hilo
wa Mikoa na kanda iliokuwa ikifanyika leo Jijini Arusha.
Mhandishi Seya kama shirika wako kwenye mikakati ya kuboresha
zaidi utendaji wake kwa viwango vya kimataifa 
vya  umeme ambapo umeme unatakiwa
kutokatika kabisa na kama utakatika ukatike mara nne kwa mwaka na mkakati wa
kutekeleza hayo umeanza leo katika kikao hicho.

Anasema wamekuwa wakiamini kuwa kikao hicho ni sehemu ya
mwarobaini wa tatizo la umeme kukatikati mara kwa mara  na kwamba wahandisi hao  wameshakusanya matatizo yote na wapo hapo
kuyapatia ufumbuzi.

“dhana kamili ya
semina hii ni moja ya kazi ambayo wahandisi hawa watafanya ni kuhakikisha
kwamba umeme haukatiki kabisa kwa sababu umeme unavyokatika hata kwa dakika
moja ni hasara kubwa sana, kwanza kabisa umeme ukikatika unailetea serikali
hasara kwani inakosa pesa, kwa upande wa viwanda vyetu navyo vinapata hasara
kwa mfano kiwanda cha kutengeneza plastiki umeme ukikatika ghafla kama
wanaendelea kuzalisha wanakuwa wameharibu 
matirio yale waliokuwa wanatengenezea kwa hiyo hii itachangia kufukuza
wawekezaji wa viwanda,”amesema.


Amesema kuwa wanataka kuhakikisha kila mwananchi anapokea na
kunufaika na umeme wa uhakika lakini pia katika sera yetu ya Tanzania ya
viwanda haiwezi kufanyakazi vizuri kama umeme utakuwa sio wa uhakika ,na pia
kama umeme hautakatika mara kwa mara pia tutawavutia wenye viwanda kuja
kuwekeza hapa nchini kwetu  na wakija
kuwekeza serikali yetu itaongeza mapato , na pia ajira zitaungezeka kwa
wananchi wetu.

Kwa upande wa muhandisi Mahende Mgaya meneja mwandamizi wa
usambazaji  wa shirika la umeme Tanzania
anasema kuwa wamechukua kumbukumbu za chanzo cha kukatika umeme za kuanzia
mwaka 2015 iliopita wakazichakata na kujua tatizo ni nini na baada ya hapo
wakatengeneza mkakati ambao wameugawa kwa awamu tatu ambapo  awamu ya kwanza wataangalia tatizo, watalifanyia
kazi  na mwisho watahakikisha tatizo
limeisha kabisa.