Meneja tcra kanda ya ziwa afanya warsha na waandishi wa habari mkoa wa shinyanga

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mamlaka  ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)  imetoa warsha kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuwakumbusha kuhusu wajibu  wa kuzingatia miiko na maadili ya kazi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi.

Akiwasilisha mada kuhusu maana na majukumu ya mamlaka ya TCRA, Meneja  wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kanda ya ziwa Mhandisi Imelda Salumu pamoja na mambo mengine amewahimiza waandishi wa habari kuwahamasisha watanzania kuingia kwenye Uchumi wa kidijitali ili kuendelea kunufaika na fursa mbalimbali.

Amesema Sekta ya Mawasiliano imeendelea kukua na kufungua fursa mbalimbali hivyo amewasisitiza waandishi wa habari kuwahamasisha watanzania kuingia kwenye Uchumi wa kidijitali pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

“Tujue kwamba tupo kwenye ulimwengu wa kidijitali na uchumi wa kidijitali Dunia yote kwa sasa hivi iko huko na kila nchi iko kwenye nafasi tofauti kulingana na sera, sheria zilizoko kwenye nchi husika sisi pia tuko huku yaani sisi TCRA tupo kama dereva au kama nahodha tunaendesha hivyo vyombo mbalimbali vya kuwapeleka watanzania kwenye uchumi wa kidijitali lakini hatuwezi kufanya hicho kitu peke yetu tunahitaji wadau wote waelewe kwamba hata mwananchi wa kawaida kama anataka kupata huduma kwa nini ahangaike mara asafiri atumie nauli yake apoteze muda kufuata huduma sehemu furani tunataka hiyo huduma aipate mtandaoni tu”.

“Mitandao ya kijamii imejitokeza na kuendelea kuwa vyombo vya kusambaza habari na taarifa mbalimbali imerahisisha mawasiliano kwa watumiaji kupata habari kwa wakati ni vyema sasa waandishi wa habari mkaendelea kujilinda kwa kuepuka kusambaza habari au taarifa za uongo na uzushi”.amesema Mhandisi Imelda

“Sekta ya mawasiliano nchini inahusisha miundombinu, utoaji na matumizi ya huduma na bidhaa katika sekta ndogo za simu na intaneti, utangazaji na post, huduma za mawasiliano ni za msingi katika maisha ya wananchi kijamii, kiuchumi na kisiasa maana mawasiliano yanawezesha na kuhimili sekta nyingine kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kutoa mchango mkubwa sana katika uchumi wa moja kwa moja na kwa kupitia sekta za Elimu, Afya, Kilimo, Biashara, Ajira, mabenki, utalii uwekezaji na sekta nyingine zote kama nyenzo za uwezeshaji katika kuongeza ufanisi wa kiutendaji”. amesema Mhandisi Imelda

Aidha Meneja  wa TCRA kanda ya ziwa Mhandisi Imelda Salumu ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi wote kuwa kesi mbalimbali za uhalifu mtandaoni ikiwemo wizi na utapeli zinapaswa kupelekwa kwenye vituo vya jeshi la Polisi ambao ndiyo wenye jukumu la kushughulikia kesi hizo na kwamba TCRA haishughulikii kesi za namna hiyo.                                          

Akiwasilisha mada iliyohusu maadili na kanuni za utangazaji mwandishi wa habari mwandamizi Bwana Edwin Soko amesema usalama wa mwandishi wa habari unategemea zaidi uzingatiaji wa miiko na maadili katika kazi yake.

Soko amesisitiza kuhusu uandishi wa habari unaozingatia ukweli,usawa,na mizania kwa pande zote zinazohusika.

“Sisi waandishi wa habari tunatakiwa tufanye nini kwenye miiko na maadili yetu, vyombo vya habari kwanza kabisa tunatakiwa turipoti habari zetu kwa ukweli na usahihi kwahiyo msingi wa kwanza ni kuwa wakweli tuhakikishe maudhui yetu hayatuletei shida, maudhui yetu yakiwa yana usahihi na yana mizania tutakuwa salama zaidi lakini vile vile tuwasilishe jambo ambalo linamantiki ya kuwasilishwa”.amesema Soko

Kwa upande wake afisa habari na mawasiliano wa TCRA Bwana Robin Albert Ulikaye amesema kuelekeza uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ni vema waandishi wa habari kuendelea kuzingatia kanuni za uchaguzi wakati wa kutengeneza maudhui.

Ameonya kuhusu uandishi wa habari zinazochangia kuchochea chuki katika jamiii,na badala yake kujikita kwenye maudhui yanayozingatia maadili  na miiko.

Takribani waandishi wa habari 55 kutoka Wilaya za Kishapu, Kahama na Shinyanga wameshiriki katika warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hotel ya Empire mjini Shinyanga.

Meneja  wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kanda ya ziwa Mhandisi Imelda Salumu akizungumza kwenye warsha hiyo leo Aprili 9,2024.

Meneja  wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kanda ya ziwa Mhandisi Imelda Salumu akizungumza kwenye warsha hiyo leo Aprili 9,2024.

 

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru akiishukuru TCRA kwa kuratibu warsha hiyo ambayo ni chachu kwa waandishi wa habari.