Mhe ikupa: wenye ulemavu wajumuishwe katika masuala ya ukimwi


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
(Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akisalimiana na baadhi ya watendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wakati wa ziara yake
wilayani hapo ili kukagua utekelezaji wa masuala ya Ukimwi katika Wilaya
hiyo Oktoba 2, 2019.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa
akizungumza wakati wa kikao cha kupokea taarifa za wilaya hiyo wakati wa
ziara yake ya kukagua na kuangalia shughuli za utekelezaji wa masuala
ya Ukimwi wilayani hapo..
Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akiuliza
jambo kwa Mratibu wa Kudhibiti masula ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo
Herieth Nyangasa (hayupo pichani)  wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi
wa Utafiti na Tathimini kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini
(TACAIDS) Dkt.Jerome Kamwela akifafanua jambo kuhusu masuala ya ukimwi
nchini kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella
Ikupa wakati wa kikao hicho.
Mratibu
wa Kudhibiti masula ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo Herieth Nyangasa
akifafanua kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala ya
ukimwi kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe.
Stella Ikupa wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya wilaya alipotembelea
Oktoba 2, 2019.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa
(katikati) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab (wa
pili kutoka kulia waliokaa), Katibu Tawala wa wilaya hiyo Desderia Haule
(wa kwanza kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya
kumaliza kikao katika ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo Oktoba 2, 2019. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

NA.MWANDISHI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masula ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa ameuasa
uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kushirikisha kundi la wenye
ulemavu katika masuala ya UKIMWI ili kuhakikisha jamii nzima inapata
elimu na huduma ya masuala hayo.
Ametoa kauli hiyo oktoba 2, 2019
wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
mkoani Tanga alipofanya ziara yake ya siku tatu mkoani hapo ili
kutembelea na kukagua shughuli zinazotekelezwa wilayani hapo kuhusu
masuala ya UKIMWI.
Alieleza kuwa kundi la wenye
ulemavu limekuwa nyuma kwa muda mrefu katika kujumuishwa hususan katika
masuala ya elimu na huduma za kijamii hivyo ni lazima kuzingatia
mahitaji yao katika kuendelea kuwapa elimu na huduma za masuala hayo ili
waweze kunufaika na huduma ili kupunguza na kuondoa maambukizi mapya
katika mkoa mzima wa Tanga.
“Ni vyema kuhusisha kundi la wenye
ulemavu katika upatikanaji wa huduma za masuala ya Ukimwi kwa
kuzingatia kundi hili limekuwa likisahaurika na kutofikiwa kama yalivyo
makundi mengine,”alieleza Mhe.Ikupa
Aliongezea kuwa miongoni mwa
mikakati ya Halmashauri ni vyema kuwa na mipango madhubuti ya
kuhakikisha huduma za masuala ya Ukimwi ikiwemo, utoaji elimu juu ya
mabadiliko ya tabia na kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, kuwashirikisha
katika program mbalimbali zinazojikita katika kuimarisha mifumo utoaji
wa elimu ya masuala ya watu wanaoishi na VVU na mikakati ya kusaidia
makundi hayo.
Alifafanua kuwa, kwa kufanya hivyo
itasaidia kupungua kwa masuala ya ubaguzi katika jamii ili kuwa na
usawa na haki kwani wenye ulemavu wanastahili kupewa huduma sawa katika
jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab alieleza kuwa wameendelea kuwafikia watu
wenye ulemavu katika huduma za upimaji, utoaji wa huduma za dawa na
kuahidi kuendelea kuwajumusha katika shughuli zote zinazohusu masuala ya
ukimwi ili kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na tisini tatu (909090).
“Tunakushukuru kwa kuendelea
kuunga mkono jitihada zetu na kukuahidi tutatekeleza maagizo yako ikiwa
ni pamoja na kutenga bajeti zinazojumuisha mahitaji maalum ya wenye
ulemavu, kuwapatia elimu, kuwafikia na kuendelea kuwashirikisha katika
program mbalimbali za kimaendeleo,”alisema Mwanashaa.
Naye Mratibu wa Kudhibiti masula
ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo Herieth Nyangasa alieleza kuwa hali ya
maambukizi kipindi cha mwaka 2018 ni asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.6
kwa mwaka 2017 ambapo imechangiwa na jitihada zinazofanywa na Serikali
katika kuwafikiwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili kuhakikisha
maambukizi mapya yanapungua.
“Zipo jitihada nyingi zimefanyika
kuhakikisha wanapunguza hali ya maambukizi mapya na kuwapatia huduma
watu wanaoishi na VVU ikiwa ni pamoja na wilaya kuwa na vituo 445 vya
kutolea huduma ya ushauri nasihi na upimaji wa VVU, vituo 20 vya upimaji
kwa hiari, vituo 38 upimaji kwa ushawishi na vituo 45 vya huduma ya
kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,”Alesema
Nyangasa.
Kwa upande wake Mratibu wa
kudhibiti Ukimwi Wilayani humo Dkt. Yahaya Mbura alieleza changamoto
zinazokwamisha jitihada za serikali katika kuwahudumia watu wanaoishi na
virusi vya ukimwi kuwa ni pamoja na tatizo la  utoro wa watumiaji wa
dawa za kufubaza Virusi vya ukimwi ambapo alieleza imechangia kwa kikasi
kikubwa kudhoofisha jitihada hizo.
“Hadi sasa tuna ripoti za utoro
kwa wanaotumia dawa wapatao 388 na hii imechangiwa na changamto za
miundombinu kipindi cha mvua, umbali wa vituo kutoka katika makazi yao
pamoja na uwepo wa imani potofu kuhusu matumizi ya dawa
hizo,”alisisitiza Dkt. Yahaya.
Aliongezea kuwa pamoja na
changamoto hiyo, tayari zaidi ya watoro 212 walifanikiwa kuwarejesha
katika huduma za upatiwaji wa dawa na kuendelea kutumia dawa.
AWALI
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ni
moja kati ya Halmashauri 11 zilizopo Mkoa wa Tanga yeye jumla ya hekta
za mraba 1,974 na jumla ya wakazi 204,461 kwa mujibu wa sensa ya mwaka
2012 ambapo kati yao wanawake ni 103,618 na wanaume ni 100,843.Aidha ina
jumla ya Kaya 47,920 yenye Tarafa 4, kata 37, vijiji 126 na Vitongoji
494 ambapo wilaya hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa
ajili ya kutekeleza afua za VVU na UKIMWI hasa zisizo za kitabibu.Wadau
hao ni pamoja na SWAAT, SHDEPHA, WORLD
VISION,KONGA,SHIVYAWATA,ZICOSAD,TIWAMWE, AMREF, AWCYS, MKUTA pamoja na
BAKWATA.