Mkuu wa mkoa wa shinyanga mhe. christina mndeme atembelea uwanja wa ndege ibadakuli, ofisi ya mwendesha mashtaka na hospitali ya rufaa ya mkoa wa shinyanga

Serikali Mkoa wa Shinyanga imesema
itaendelea kushughulikia changamoto zilizopo katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa
wa Shinyanga ikiwemo ujenzi wa majengo mapya pamoja na uboreshaji wa
miundombinu ya barabara ili kuepusha usumbufu uliopo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Bi. Christina Mndeme baada ya kupokea changamoto katika taarifa fupi
iliyosomwa na mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga
iliyopo Mwawaza Dkt. Luzila John leo Jumanne Oktoba 31, 2023.

Dkt. Luzila ametaja baadhi ya changamoto
zinazoikabili Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ikiwemo upungufu wa
watumishi, ukosefu wa Mochwari pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara
inayotoka mjini kuendelea katika Hospitali hiyo ya rufaa.

“Tunachangamoto
ya uchache wa majengo  Maabala imepelekwa
ambako siyo sehemu yake kwahiyo wagonjwa wanapata wakati mgumu kwa ajili ya
ubali wa majengo haya, upungufu wa watumishi tunaupungufu wa asilimia 47,
changamoto nyingine ni kuharibika kwa barabara ambayo haijajengwa kwa kiwango
cha lami imekuwa ni usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na watumishi gali zinaharibika
mara kwa mara kwa sababu ya ubovu wa barabara tunakuomba kama ikiwezekana jambo
hili liharakishwe ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga”

amesema Dkt. Luzila

“Tunaishukuru
sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa
tiba pamoja na kutuletea watumishi”.

Dkt. Luzila amesema Hospitali ya rufaa
ya Mkoa wa Shinyanga inatoa huduma za kimatibabu kwa asilimia mia moja pamoja
na huduma za matibabu ya wagonjwa wa ndani na wa nje zinafanyika ikiwemo huduma
za kliniki za kibingwa za magonjwa ya ndani upasuaji wa watoto pamoja na
magonjwa ya akina mama kwa siku zote za wiki.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina
Mndeme amesema kipaumbele cha serikali ya Mkoa wa Shinyanga ni kuitengeneza
barabara inayotoka Mwawaza hadi kata ya Ndala kwa kiwango cha lami ili kuondoa
usumbufu wa wagonjwa na wakazi wa Mkoa wa Shinyanga.

“Barabara
hii ambayo ni kilometa tatu kutoka Ndala kuja Mwawaza ni changamoto ambayo
tunaishughulikia napenda kuahidi kwamba barabara hii tunakwenda kuitengeneza
kwa kiwango cha lami malengo tufike mpaka kijijini Mwawaza lakini tunaanza
kwanza kuishia hapa Hospitali ya rufaa na tutaanza na mitalo hicho ni
kipaumbele cha serikali ya Mkoa kuhakikisha kwanza fedha tutakayoipata ni
kujenga hizi kilometa tatu haziwezi kutushinda kwahiyo suala hili
tunalishughulikia ili tuondoe changamoto iliyopo ya ubuvu wa barabara”.amesema

 RC Mndeme.

Mhe. Mndeme amewataka watumishi wa
Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa elimu ya afya kwa
wananchi ili kuepukana na athari mbalimbali ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza,
magonjwa ya kisukari pamoja na magonjwa na shinikizo la damu.

Amewasisitiza watumishi hayo kufanyakazi
kwa kuzingatia sheria, taratibu na maelekezo ya wizara hiyo ambapo  amemuagiza mganga mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Dkt. Yudas Ndungile, mganga mfawidhi Dkt. Luzila John pamoja na wakuu wa idara
kusimamia upotevu na wizi wa dawa na vifaa tiba.

RC Mndeme amewapongeza watumishi wa
Hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga huku akiwakumbusha kuendelea
kutumia lugha nzuri na kuepuka kuongea na simu au kuchezea simu wakati wa
kumhudumia mgonjwa.

Aidha mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Christina Mndeme katika ziara yake leo ametembelea ujenzi wa ofisi ya mwendesha
mashtaka Mkoa wa Shinyanga ambapo thamani ya mradi huo ni zaidi ya shilingi
Bilioni mbili mradi na kwamba umefikia asilimia 60 ya ujenzi na  unatarajiwa kukamilika Disemba 28,2023.

Mkuu wa Mkoa huyo pia ametembelea ujenzi
wa kiwanja cha ndege katika kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga huku
akiagiza ukamilike kwa wakati ili uanze kutumia na kufikia malengo
yaliyokusudiwa na serikali.

Awali akisoma taarifa fupi ya utekelezaji
wa upanuzi wa kiwanja cha ndege  Mkoa wa
Shinyanga, meneja TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi amesema
ujenzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 4.5 mpaka sasa.

“Muda
wa mkataba ni miezi 18 tarehe ya kumaliza mradi huu ni Novemba 20,2024 mkandarasi
yupo eneo la mradi na hatua za utekelezaji wa kazi unaendeleo ukiwa umefikia asilimia
4.5, ujenzi wa kiwanja hiki cha ndege utawapunguzia ada wananchi wa Mkoa wa
Shinyanga na Mikoa jirani tunatarajia uwepo wa kiwanja hiki utafungua fursa za
uwekezaji katika Mkoa wetu wa Shinyanga napenda kukuhakikishia kuwa matarajio
yetu mkandarasi atamaliza kazi ndani ya muda uliopangwa”
.amesema
Mhandisi Ndirimbi

Kwa upande wake meneja miradi wa kampuni
ya CHICO Shi Yinlei na mhandisi mkazi wa mradi huo Nasser Elgohary  wamesema mradi huo utakamilika kwa wakati huku
wakiahidi kutoa kipaumbele kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga katika suala la
ajira.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina
Mndeme ameendelea na ziara zake ambapo leo ametembelea na kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga ziara hiyo imehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga
kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi pamoja na mkuu wa Wilaya ya Shinyanga
Mhe. Johari Samizi.

 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina
Mndeme akisalimiana na viongozi mbalimbali leo Oktoba 31,2023 baada ya kuwasili
katika eneo la uwanja wa ndege wa Mkoa wa Shinyanga unaojengwa kata ya
Ibadakuli.