Mvua yabomoa nyumba 20 katavi



Zaidi ya nyumba 20 katika kijiji cha Kamsanga B, kilichopo Kata ya
Mnyagala Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, zimebomoka huku zingine
zikiwa zimeezuliwa mapaa, kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali
na kujeruhi watu watatu.


Akizungumzia tukio hilo Mtendaji wa Kijiji hicho Mwikobe Saimon, amesema
mpaka sasa nyumba 17 zimebomoka na nyumba 20 zimeezuliwa mapaaa.


“Jana majira ya jioni mvua iliyoambatana na upepo mkali ilianza kunyesha
na ikaezua mapaaa na tulifika kuangalia namna ya kuwanusulu ila nyumba
ishirini mapaa yake yalikuwa yamedondoka na nyumba 17 ndiyo zilikuwa
zimebomoka kabisa” amesema Mtendaji wa Kijiji hicho Mwikobe Saimon.


Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Salehe Mhando, amefika kijijini hapo na
kutoa pole kwa waathirika wa upepo huo, ambapo amesema kuwa Serikali
itaandaa utaratibu maalum wa kuwasaidia.

 “Kwenye suala la ujenzi inabidi tuendelee kuelimishana ili tuweze kuweka
vizuri, mfano nyumba ikiwa haijafungwa lenta ikipata misukosuko
inabomoka” amesema Mkuu wa Wilaya.