Mvua yaua watu 9 sengerema jijini mwanza

Watu
tisa wa familia mbili tofauti katika Kata Yanyatukala Wilayani
Sengerema, mkoani Mwanza wakiwemo wanawake wanne pamoja na watoto watano
ambao nyumba zao ziko kwenye mkondo wa mto wamefariki, baada ya
kusombwa na maji ya mvua.

 

Mvua
hiyo iliyoanza kunyesha majira ya asubuhi, ilinyesha na kusababisha
maafa kwa baadhi ya nyumba ambazo zipo pembezoni mwa mto na kupelekea
nyumba hizo kusombwa na maji, kusababisha vifo vya watu tisa pamoja
daraja kukatika na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano.

Mkuu
wa wilaya hiyo Dkt. Emmanuel Kipole amewataka wananchi wanaoishi katika
maeneo hayo kuyapisha na kwenda kuishi katika maeneo ya muda, ambayo
tayari serikali imeyabainisha ili kuepusha madhara zaidi.

Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza John Mongella  ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mwanza, amewataka wakazi wa maeneo hayo
kuchukua tahadhari ili kuepusha kupoteza maisha ya wananchi wengine
zaidi..

Miili
yote ilikuwa imepatikana na imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Sengerema, baada ya zoezi la uokoaji kufanywa na wananchi kwa
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutumia nyavu na kamba.