Mwekezaji kutoka malaysia kuwekeza mradi wa dola bilioni 2.5 simiyu

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mwekezaji Azhar Malik kutoka Nchini Malaysia ameonesha nia ya kuwekeza
kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.5 katika mradi mkubwa eneo la
pori la akiba la Kijereshi na Ziwa Victoria wilaya ya Busega Mkoani
Simiyu, sehemu ya uwekezaji huo ikiwa ni katika ujenzi wa hoteli ya
kitalii, usafirishaji, utamaduni na maeneo mengine yatakayoimarisha
utalii na kutoa ajira kwa wananchi.

Mwekezaji ambaye amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe.
Dkt. Ramadhan Dau amesema ikiwa kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa
ikiwemo mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari
2020, huku akisisitiza kuwa utatekelezwa bila kuathiri ikolojia na
mazingira ya uhifadhi.

“Nashukuru kwa ushirikiano nilioupata kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu,
pia namshukuru Balozi Dau kwa namna alivyolisimamia jambo hili tangu
likiwa wazo mpaka sasa tunapoelekea kwenye utekelezaji niwaahidi tu kuwa
pale pande zote zitakapofanya maamuzi mikataba ikisainiwa kwa mujibu wa
sheria, mwakani mwezi Januari tutaanza utekelezaji,”alisema Malik

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhan
Dau amepongeza uongozi wa Chama na Serikali kwa utayari walioonesha,
akisisitiza ushirikiano wa viongozi hao na taasisi zote za Serikali
zinazohusika, ili mambo yote muhimu yanayohitajika kufanikisha uwekezaji
huo yafanyike mapema  kuanzia mwezi Januari kazi ianze.

“Kwa kasi na namna tulivyoanza lile lengo tulilojiwekea kwamba ikifika
Januari 2020 mambo yote yanayohusiana na taratibu na  kusaini mikataba,
yanapaswa yawe yamekamilika na wataalam waje site (eneo la mradi) waanze
survey (utafiti) watengeneze master plan(mpango kabambe), ili kabla ya
mwezi Juni 2020 hili jambo liwe limeanza,” alisema Balozi Dau.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Uwekezaji huu
utaupambanua Mkoa wa Simiyu, Kanda ya Ziwa na kuupambanua utalii kwenye
uso wa dunia, ambapo amebainisha kuwa mradi huu utajibu mahitaji mengi
kwenye ajira na kukua kwa maendeleo ya ukanda huo.

Kwa upande wao Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori (TAWA) wameahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huu
unafanikiwa.

Mradi huu wa uwekezaji katika sekta ya utalii wilayani Busega
utatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kugharimu
takribani dola bilioni 500 na mpaka kukamilika kwake utagharimu dola za
Kimarekani bilioni 2.5