Na Seif Mangwangi, Arusha
RUSHWA na ufisadi vimeelezwa kuwa janga kubwa katika nchi nyingi barani Afrika na ambalo limekuwa likisababisha hasara kubwa ya upotevu wa mapato ya zaidi ya Dola bilioni 50 kila mwaka barani humo huku nchi hizo zikiogelea kwenye umaskini mkubwa.
Hayo yameelezwa leo Novemba7, 2024 jijini Arusha na Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Umoja wa Afrika Dhidi ya Ufisadi (AUABC), Seynabou Ndiaye Diakhate katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mdahalo wa 8 wa umoja wa Afrika kujadili ulinzi wa wadau wa mapambano dhidi ya kupinga rushwa na ufisadi barani Afrika.
Seynabou amesema rushwa na ufisadi vimekuwa vikiendelea kukififisha maendeleo ya nchi nyingi barani Afrika huku wala rushwa wakiendelea kutamba kufuatia wananchi kutotoa taarifa kwa mamlaka husika wakiogopa ulinzi wa taarifa watakazotoa.
Amesema mwaka jana 2023 wakati wa kuazimisha miaka 20 tangu umoja wa Afrika kupitisha Mkataba wa Umoja a Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (AUCPCC), na mapitio ya safari ya AUCPCC kulionyesha kuwepo kwa maendeleo, hatua , mafanikio yaliyopatikana katika uanzishwaji huo pamoja na changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.
“Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa tangu kuanzishwa kwa AUCPCC ni pamoja na mbinu duni za ulinzi wa watoa taarifa. Ili kukabiliana na changamoto hizi baadhi ya maeneo muhimu yalibainishwa kuwa maeneo ya kuzingatia bodi ikiwemo kusaidia nchi wanachama uanzishaji wa taratibu za kuwalinda watoa taarifa na mashahidi,”amesema.
Amesema ni muhimu changamoto za uanzishwaji wa taratibu za kulinda watoa taarifa zikafanyiwa utekelezaji wa haraka ambapo amesema kufichua daima imekuwa kipengele muhimu cha juhudi za kupamba na ufisadi.
Kifungu cha 5(5) cha AUCPCC kinazitaka Nchi wanachama kutekeleza hatua za kulinda watoa taarifa na mashahidi ikiwa ni pamoja na kulinda utambulisho wao na pia ibara ya 5(6), inaangazia umuhimu wa taratibu zinazoruhusu wananchi kukemea rushwa bila kuogopa.
Seynabou amesema pamoja na juhudi zote za bodi hiyo kuhakikisha nchi za Afrika zinapambana na rushwa, suala la utawala bora linapaswa kutiliwa msisitizo kwa kuwa ndio msingi wa haki za binaadam katika Taifa lolote.
“Tukiwa kama washirika tunaofanyakazi pamoja kuhakikisha tuna bara ambalo ni la haki, sote tunakubaliana kwamba haki za binaadam na haki za kijamii na kiuchumi zote zimeunganishwa kwa kina ndani ya juhudi zetu za kupambana na ufisadi,”amesema na kuongeza:
“Hata hivyo haki za binaadam haziwezi kufurahiwa bila kuwepo kwa utawala bora sanjari na uanzishwaji wa taasisi zinazoweza kutoa haki na kupambana na uadilifu na taasisi hizo zinapaswa kuwa na uwiano wa pamoja katika kupinga ufisadi,”amesema.
Ametoa wito kwa washiriki wa mdahalo huo wa siku mbili unaoshirikisha wadau kutoka taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGO’S), pamoja mashirika ya kimataifa pamoja na wawakilishi wa taasisi za kiserikali zinazopambana na masuala ya rushwa kuchangia mada kuhusu mafanikio na changamoto mbalimbali za kuanzishwa mifumo madhubuti ya kudhibiti ufisadi pamoja na kulinda watoa taarifa.