Ni marufuku kulisha mifugo vyakula vibovu-serikali

 

Mkurugenzi
wa Uendelezaji Malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe
Rwiguza (kulia) akifafanua jambo mbele ya wataalam wa ukaguzi wa malisho
na rasilimali za vyakula vya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye
kiwanda cha kusindika chakula cha mifugo kinachojulikana kama “Musoma
Animal Feed” kilichopo mkoani Mwanza leo

Meneja
wa Kiwanda cha “Musoma Animal Feed” Bi. Maajabu Musa (mwenye kilemba
cheusi) akitoa maelekezo ya namna chakula cha mifugo kinavyotengenezwa
kiwandani hapo mbele ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Mikoa ya Mwanza, Arusha,
Shinyanga na Arusha wakati wa ziara yao waliyoifanya leo (13.11.2020)
mkoani Mwanza.


……………………………………………………………………………….

Serikali
imepiga marufuku matumizi ya vyakula vilivyopoteza ubora wa kutumiwa
na binadamu na kutumiwa kama vyakula vya mifugo kabla ya kuthibitishwa
kwanza na wataalam wa maabara ya mifugo.

Hayo
yamesemwa leo (13.11.2020) na Mkurugenzi wa Uendelezaji Malisho na
rasilimali za vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza ikiwa ni sehemu ya
kuhitimisha mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo
kutoka mikoa ya Mwanza,Shinyanga, Singida na yaliyofanyika Mkoani
Mwanza.

“Kumekuwa
na mazoea ya vyakula ambavyo vimeshapoteza ubora wa matumizi ya
binadamu kutumika kama vyakula vya mifugo hivyo ninapenda kutumia fursa
hii kutoa wito kwa wafugaji, wazalishaji na taasisi mbalimbali
zinazojihusisha na uzalishaji wa vyakula vya binadamu kuwa ni marufuku
kutumia vyakula hivyo bila Wizara yenye dhamana kuwa na taarifa na
kujiridhisha kitaalam kama chakula hicho kinafaa au la” Amesisitiza Dkt.
Rwiguza.

Aidha
Dkt. Rwiguza amebainisha madhara yanayoweza kumpata mtu ambaye atatumia
mazao ya mfugo uliokula vyakula hivyo kuwa ni pamoja na kupatwa na
magonjwa mbalimbali kama vile Kansa.

Upande
wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na rasilimali
za vyakula vya Mifugo Bw. Roggers Shengoto amesema kuwa mafunzo hayo
yamekuwa na manufaa makubwa kwa sababu sehemu zaidi ya asilimia 90 ya
wataalam walioalikwa walishiriki.

“Pia
kupitia mafunzo haya tumegundua kuwa bado kuna haja ya Halmashauri za
vijiji kutenga maeneo ya malisho ya mifugo na pia wazalishaji na wauzaji
wa vyakula vya mifugo bado hawazingatii sheria na kanuni za kufanya
shughuli hizo hivyo tuna imani wataalam hawa wataenda kuleta mabadiliko
katika maeneo yote yenye changamoto kwa mfugaji” Ameongeza Shengoto.

Nao
baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa wamenufaika na yote
waliyofundishwa ambapo wameahidi kuyafanyia kazi na kubadilisha utendaji
wao pindi wakirejea kwenye vituo vyao vya kazi.

“Kwa
mfano, zamani nilikuwa naenda kwa mdau kama Mkaguzi na nilikuwa natumia
lugha ya mamlaka lakini kupitia mafunzo haya nimefundishwa kumfuata
mdau kama rafiki na kuzungumza naye kwa lugha ya kawaida” Amesema mmoja
wa washiriki Veronica Ngoso.

Takribani
wakaguzi 129 nchi nzima wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni.