Nmb tawi la mirerani wazindua mikopo ya afya loan


Meneja wa benki ya NMB Tawi la
Mirerani Allan Kombe (katikati) na wadau na watumishi wa benki hiyo
wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye tafrija ya wiki ya huduma kwa
wateja.  


Watumishi wa benki ya NMB Tawi la
Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye maadhimisho ya
wiki ya huduma kwa wateja.


Meneja wa benki ya NMB Tawi la
Mirerani, Allan Kombe (kushoto) akiwa na wadau na watumishi wa benki
hiyo kwenye tafrija ya wiki ya huduma kwa wateja. 

Na mwandishi wetu, Mirerani 
 

Wafanyakazi wa benki
ya NMB Tawi la Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamezindua
wiki ya huduma kwa wateja kwa kutangaza mpango mpya wa mikopo ya ‘Afya
Loan’. 
 

Meneja wa NMB Tawi la
Mirerani, Allan Kombe akizungumza na wadau na wafanyakazi wa benki hiyo
kwenye tafrija ya wiki hiyo alisema Afya Loan ni huduma mpya maalum ya
mikopo kwa watu au taasisi binafsi. 
 

Kombe alisema Afya
Loan ina lengo la kuwakopesha wadau binafsi wenye maduka ya dawa,
maabara, zahanati na vituo vya afya vya watu binafsi. 
 

Alisema lengo la
kuanzishwa kwa mikopo hiyo ya ‘Afya Loan’ ni kwa ajili ya kuimarisha
huduma hizo za afya zinazotolewa na watu binafsi au taasisi binafsi. 
 

“Mpango huo wa ‘Afya
Loan’ utakuwa endelevu na wiki hii ya huduma kwa wateja itaendelea kwa
muda wote wa mwezi huu wa Octoba,” alisema Kombe. 
 

Ofisa Tarafa ya
Moipo, Joseph Mtataiko aliwapongeza wafanyakazi wa benki ya NMB Tawi la
Mirerani kwa kutoa huduma zao ipasavyo kwa wateja wanapofika kupata
huduma za kibenki. 
 

Mtataiko alisema
watumishi wa serikali, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wachimbaji
madini na watu wa kada zote za Mirerani wanaopata huduma kwenye benki
hiyo wanapongeza huduma nzuri zinazotolewa na benki hiyo. 
 

Meneja wa huduma kwa
wateja wa benki ya NMB Tawi la Mirerani, Bahati Nelson aliwakaribisha
wadau wote wa benki hiyo kufika ofisini kwao ili wapatiwe huduma. 
 

Bahati alisema benki
ya NMB Tawi la Mirerani ipo pembeni ya barabara kuu ya
Mirerani-Okresumet mbele kidogo ya kituo cha polisi Mirerani.