Polisi yachunguza kifo cha mwanafunzi wa darasa la sita kutoa mimba

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, amesema kuwa bado
wanachunguza chanzo kufuatia kifo cha Mwanafunzi wa darasa la sita
katika Shule ya Msingi Mtumbatimaji, anayedaiwa kufariki baada ya kutoa
mimba.
Akizungumza na EATV&EA Radio Digital leo Novemba 8, 2019, Kamanda
Maigwa amesema kuwa binti huyo alifikishwa hospitalini akiwa tayari
anavuja damu, hivyo bado wanafanyia uchunguzi kwa sababu hata mama mzazi
wa binti huyo bado hajatoa maelezo ya kina.
“Ni kweli hili tukio limetokea na bado tunachunguza lakini alipelekwa
hosptali na wazazi wake akiwa tayari anavuja damu na baada ya kukaa
hospitali akiendelea na matibabu akafariki, mama yake wakati anajaribu
kuhojiwa alikuwa anazimia sasa ni masuala ya kibindadamu inabidi
kumuacha mtu atulie”, amesema Kamanda Maigwa.
Aidha Kamanda Maigwa ameongeza kuwa mara baada ya uchunguzi wa tukio
hilo kukamilika, Jeshi la Polisi litatoa taarifa ya kina kuhusu kifo
hicho.
Chanzo – EATV