Rais magufuli afunguka mazito kuhusu uhuru wa kisiasa

Rais
John Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) amesema, uhuru wa kisiasa hauna maana kama nchi za Afrika
zitaendelea kuwa tegemezi kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Novemba
2019, wakati akifungua Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za
Afrika na NORDIC, jijini Dar es Salaam.
“Viongozi wengi wa Afrika tumetambua
kuwa, mustakabali wa Bara letu uko mikononi mwetu, na kwamba uhuru wa
kisiasa hauwezi kuwa wa maana sana, endapo mataifa yetu yataendelea kuwa
tegemezi kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.

Na kwamba, mataifa ya Afrika hayawezi
kuwa Huru wa kujiamulia masuala yake, iwapo yataendelea kuwa ombaomba.
Na kuwa, viongozi wa Bara hilo jukumu lao ni kutafuta ukombozi wa
kiuchumi.

“Hatuwezi kuwa na Uhuru wa kujiamulia
mambo yetu wenyewe, endapo mataifa yetu yataendelea kuwa ombaomba.
Kutafuta ukombozi wa kiuchumi ndio jukumu la viongozi wa Afrika. Hata
Mwalimu Julius Nyerere alisema, ukombozi wa Afrika ni kujikomboa
kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.

Pia, amesema ushirikiano wa kutoa na kupokea misaada, hauhitajiki kwa sasa, kwani sio endelevu.

“Pamoja na uhusiano mzuri na mafanikio
makubwa yaliyopatikana kwenye ushirikiano, bado tuna fursa ya kukuza
ushirikiano wetu ili kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

“Na suala hili ni muhimu kwasababu, kwa
muda mrefu ushirikiano wetu umejikita zaidi kwenye kutoa na kupokea
misaada, ushirikiano wa aina hii sio endelevu na wala hauhitajiki katika
mazingira ya sasa, “ amesema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa Tanzania amependekeza
nchi za Afrika kubadilisha ushirikiano, kutoka kwenye ushirikiano wa
kupokea misaada, kwenda kwenye ushirikiano wa kiuchumi.

“Ni lazima tubadilishe muelekeo na
kuingia kwenye uhusiano wa kisasa baina ya mataifa, ambao unajikita
kwenye uchumi kupitia biashara na uwekezaji. Diplomasia ya uchumi ndio
iwe kwenye ushirikiano kwa mataifa yetu,” ameeleza Rais Magufuli.