Polisi yawataka wakenya wanaotuhumiwa kwa ujangili kujisalimisha

Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi mkoa wa Arusha limewataka  watuhumiwa wawili wa Ujangili waliokimbilia nchi jirani ya Kenya kujisalimisha mara moja vinginevyo  nguvu itatumika kuwatafuta popote pale walipo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha,Jonathan Shana, ameyasema hayo Mei 12 ofisini kwake  alipokuwa akitoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa wawili wa ujangili.
Amesema May 10 Jeshi la polisi kwa kushirikiana na kikosi kazi kanda ya kaskazini kupambana na ujangili,walifanya msako katika kijiji cha Olosho,Enguserosambu  tarafa ya Loliondo, wilayani Ngorongoro na kufanikiwa kukamata watu wawili wakiwa na silaha moja ya kivita ya AK 47 ikiwa na risasi 12 zilizokuwa ndani ya magazine..
Amesema kuwa silaha hiyo ilipatikana baada ya kikosi kazi hicho kupata taarifa fiche kuwa kuna watu wane wawili ni watanzania na wawili ni wakenya,walionekana maeneo ya mpakani wakiwa wanajipanga kuwinda wanyama pori  adimu katika moja ya hifadhi zetuwakisadikiwa kuwa na bunduki mbili za kivita.
Amewashukuru wananchi  ambao wameendelea kutoa  taarifa  mbalimbali za uhalifu na wahalifu na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano huo.Kamanda,Shana, ameahidi  kutoa donge nono kwa mwananchi yeyote  atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa wahalifu  wanaojihusisha na uwindaji haramu ,ujambazi na uhalifu mwingine .
Kamanda Shana, ametoa onyo kwa wanaotaka kujihusisha na ujambazin na uhalifu mwingine kuacha mara moja na kusisitiza kuwa wasitumie mwanya wa ugonjwa wa Corona kufanya uhalifu ,jeshi la polisi halijalala na watafanya msako wakati wowote iwe mchana au usiku inyeshe mvua au isinyeshe iwe kiangazi au mvua au matope.
 Katika tukio lingine jeshi la polisi limemtaka Oliver Yassenti ambaye ni mkazi wa Mto wa mbu wilayani Monduli,kujisalimisha ili akatumikie kifungo chake cha mwaka mmoja alihukumiwa na mahakama ya Mwanzo ya Mto wa Mbu kutokana na kesi iliyokuwa ikimkabili ya kuiba magurudumu mawili ya gari Scania, yenye thamani ya shilingi milioni 2,400,000 .
Amesema kuwa Mtuhumiwa huyo ambae alikuwa ni mtumishi wa kituo cha mafuta cha kiitwacho Mto wa mbu service Station alishitakiwa kwa kosa la wizi na alifungwa akiwa hayupo mahakamani .Amesema siku ya tukio mtuhumiwa huyo aliiba magurudumu hayo 23 oktoba 2019 na kasha kukodi Guta na kwenda kuyahifadhi kwa Debora Joseph, anayeishi kona ya Engaruka umbali wa kilometa mbili kutoka kwenye kituo cha mafuta alichokuwa akifanyia kazi.
Amesema katika tukio hilo jeshi la polisi liliwakamata mtuhumiwa, waendesha Guta wawili pamoja na Debora ambae aliyapokea magurudumu hayo na alihukumiwa 20 Desemba 2019 ambapo katika kesi hiyo wengine watatu waliachiliwa huru na yeye alihukumiwa kifungo cha miezi 12 jela.
Kamanda, amesema kuwa katika hatua isiyokuwa ya kawaida mtuhumiwa huyo ambae hajakamatwa ameibuka na kuvitumia vyombo vya habari kwa ajili ya kutafuta huruma jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kusisitiza kwamba anamtaka ajisalimishe ili akatumikie kifungo chake.
Kuhusu ugonjwa wa Corona,amesema jeshi la polisi linachukua tahadhari zote  za kujilindana kuwalinda wateja na wahalifu waliopo mahabusu ili wasife bali wasubiri kupambana na kesi zao.