Prof.mkumbo aitaka fcc kuweka mazingira bora ya udhibiti wa ushindani wa biashara nchini

 

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.
Kitila Mkumbo,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa majadiliano ya
Mpango Mkakati wa tano (5) wa FCC utakaoiwezesha Tume hiyo kuweka
mazingira bora ya ushindani kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi
uliofanyika jijini Dar es salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.
Kitila Mkumbo,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua
Mkutano wa majadiliano ya Mpango Mkakati wa tano (5) wa FCC
utakaoiwezesha Tume hiyo kuweka mazingira bora ya ushindani kwa
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi uliofanyika jijini Dar es
salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.
Kitila Mkumbo ameitaka Tume ya Ushindani nchini – FCC kuweka mazingira
bora ya udhibiti wa ushindani wa biashara nchini kwa lengo la kumlinda
mlaji na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Prof. Mkumbo ametoa maelekezo hayo
wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya Mpango Mkakati wa tano (5) wa
FCC utakaoiwezesha Tume hiyo kuweka mazingira bora ya ushindani kwa
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi uliofanyika jijini Dar es
salaam.

Aidha, ameipongeza FCC kwa kuandaa
Mpango Mkakati unaoakisi Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Maono,
Maelekezo na Mwelekeo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu
ya Sita.

Prof. Mkumbo pia amewatoa hofu
wafanyabiashara kwa kusema kuwa Serikali kwa sasa haiendeshi shughuli za
biashara kwa uhodhi wa dola bali kwa uhodhi wa sekta binafsi.

Amewahimiza wafanyabiashara na
wamiliki wa Viwanda kufikiria na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia
ushindani katika soko la Kijumuiya, Kikanda na Kimataifa kuliko
kuangalia soko la ndani pekee.

Prof. Mkumbo pia ametoa wito kwa taasisi zote zenye jukumu la
kuchangia FCC kufanya hivyo kwa wakati ili kuiwezesha taasisi hiyo
kutekeleza majukumu yake ya msingi bila kukwama.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema FCC ina jukumu kubwa la kuhakikisha
kuwa kuna ushindani wa bidhaa unaofuata misingi ya uhuru na haki katika
soko huria huku ikidhibiti bidhaa hafifu na kumlinda mlaji kwa ajili ya
uchumi shindani na maendeleo ya watu.

“ FCC ndio ina wajibu wa kuchagiza
maendeleo ya viwanda yanayolenga kuwa na uchumi shindani unaotokana na
bidhaa zilizoongezwa thamani na zenye ubora” Amesema Mhe. Kigahe.

Akiongea kabla ya ufunguzi, Afisa
Mtendaji Mkuu wa Tume ya ushindani (FCC) William Erio amesema mpango huo
wa tano (5)tangu kuanzishwa kwa FCC unalenga kumlinda mlaji na
kudhibiti bidhaa bandia ili kuleta ufanisi katika utendaji na kukidhi
matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla.