Rais dkt magufuli aweka rehani ajira za wakurugenzi wa halmashauri waliokopa benki, awataka waliokwisha kopa wazirejeshe kabla hawajafukuzwa kazi

AJIRA za wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa na Majiji nchini ni sawa na kusema ziko hatarini baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku Wakurugenzi  Watendaji wa Halmashauri zote
nchini kuacha  mara moja kukopa fedha kwenye taasisi za fedha kwa madai
ya kufanya miradi ya maendeleo.

Rais Magufuli amesema endapo kama kuna Mkurugenzi amekopa fedha  kwaajili ya kufanyia miradi ya maendeleo na bado hazijaanza kutumika azirudishe mapema na kama hatofanya hivyo atakuwa amejifukuzisha kazi.

Ametoa kauli hiyo Jumatano Novemba 27, 2019 wilayani Bukombe mkoani
Geita wakati akihutubia mkutano wa hadhara, Rais Magufuli ambapo amewaagiza
hao ambao wameshakopa kuzirudisha na kuvunja
mikataba waliyoingia.

“Kama kuna mkurugenzi yeyote amekopa fedha azirudishe, mwenye mamlaka ya
kukopa kwa niaba ya Serikali ni paymaster general wa Serikali ambaye ni
Wizara ya Fedha pekee.”

“Anayekopa ajiandae kutoka. Naamini Wakurugenzi wamenielewa, nimepita
Kahama Mkurugenzi ananiambia anataka kukopa kutoka TIB (Benki ya
Uwekezaji Tanzania) kwa ajili ya kujenga stendi, haiwezekani fedha za
wananchi kuchezewa, ovyo”  alisema Rais Magufuli