Rais magufuli afichua siri ya ukamataji vigogo waliopiga bilioni 1.2 za korosho

Rais
John Magufuli amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), inawashikilia viongozi wa vyama vya ushirika 92 mkoani
Mtwara kwa tuhuma za kuwadhulumu wakulima wa korosho Sh. bilioni 1.2.


Amesema fedha hizo ni malipo ya korosho katika msimu wa mwaka 2016 hadi 2017, amewaahidi wakulima hao watalipwa fedha zao.

Aliyasema hayo jana, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akiwaapisha viongozi aliowateua mwishoni mwa wiki.

“Juzi
nilikuwa Mtwara, Brigedia Jenerali Mbungo (Kaimu Mkuu Takukuru)
anafahamu tulikuta malalamiko sana ya baadhi ya watu waliodhulumiwa
malipo yao ya korosho kuanzia mwaka 2016 hadi 2017,” alisema na
kuongeza:

“Na
vilikuwa ni vyama vya ushirika 10, baada ya kumwagiza Brigedia
Jenerali, akakuta ni vyama vya ushirika 32 ambavyo vilikuwa
vinawadhulumu watu. Tulidhani walikuwa wamedhulumu Sh. milioni 80
tukakuta wamezdhulumiwa zaidi ya Sh. bilioni 1.2.”

Rais
Magufuli alisema Takukuru imeweza kuwashika viongozi wa Amcos 92 na
mpaka juzi walipokuwa wanampatia taarifa (Rais Magufuli) zilikuwa
zimerudishwa Sh. milioni 255, na kwamba zilizobakia zinaendelea
kurudishwa.