Rais magufuli amng’oa kangi lugola na thobias andengenye…. “hatuwezi kuendesha nchi kwa misingi ya ajabu…”

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola
akijadiliana jambo na aliyekuwa Kamishna Jenereli wa Jeshi la Zimamoto
na Uokoaji Thobias Andengenye hivi karibuni.Viongozi hao Wawili Uteuzi
wao umetenguliwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli leo hii kwenye hafla ya
kukabidhi nyumba za Maofisa wa Magereza Ukonga jijini Dar es salaam.


Na Elizabeth Edward, Mwananchi 

 Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye hawafai kuendelea na nyadhifa
zao kutokana na mambo waliyoyafanya.

“Nitaendelea kuwapenda lakini kwenye nafasi zenu hapana. Watanzania
mmenichagua kusimamia haki na utendaji kazi ndani ya Serikali ili kila
fedha ya Watanzania iktumike kwa mujibu wa sheria,” amesema Rais
Magufuli.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 23,
2020 katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za Jeshi la Magereza Ukonga,
jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa tume nyingi zimeundwa
kuchunguza miradi ya hovyo inayosimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Magufuli amesema kutokana na sakata hilo katibu mkuu wa wizara hiyo,
Meja Jenerali Jacob Kingu ameandika barua ya kujiuzulu na amemkubalia.
“Watu wamekosa uadilifu, hivi karibuni kulikuwa na mkataba mmoja wa
ajabu unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya zaidi ya
Sh1 trilioni. Mradi huo umesainiwa na kamishna jenerali wa Zimamoto.”
“Haujapangwa kwenye bajeti na haujapitishwa na Bunge. Wakati wa vikao na
kampuni moja ya Romania, wahusika wote wa Tanzania waliokuwa wanakwenda
katika majadiliano na kulipwa Dola 800 za posho ya vikao,” amesema
Magufuli, na kubainisha kuwa hata tiketi za ndege walilipiwa.
Amesema mkataba huo ni wa hovyo kwa sababu ili kuuvunja yaliyoanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa.
“Lugola nampenda sana ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema
Sekondari pamoja na mwili na ukubwa wake lakini katika hili hapana.
Nilitegemea hata hapa sitamkuta, nasema kwa dhati.”
“Andengenye nampenda sana, ni mchapakazi lakini kwenye hili hapana,
nilitegemea asiwepo hapa. Hatuwezi kuendesha nchi kwa misingi ya ajabu
namna hii. Yanayokwenda kununuliwa katika mkataba ni ya hovyo.”
Ameongeza, “nampongeza Kingu kwa kuwajibika na hii imempa heshima kwamba
angalau ametambua, inawezekana haya hakuyafanya yeye lakini kwa kuwa
yeye ni katibu mkuu amewajibika kwa hilo, nampongeza na nitaendelea
kumheshimu.”
Magufuli ameshangazwa mtu kusaini Sh1 trilioni wakati jukumu la kukopa fedha ni la Wizara ya Fedha.
Amesema haiwezekani watendaji kufanya mambo wanavyotaka kwa kuwa
wataipeleka nchi kubaya na kukiuka misingi na ilani ya uchaguzi ya CCM.
“Huo ndio ukweli na siku zote nitasimamia ukweli, Ndugu zangu ninajua
hili…, wapo pia ofisi ya mwanasheria mkuu, walisubiri mwanasheria mkuu
alipofiwa na mke wake wakaenda wakapitisha na kuandika kwa niaba na kwa
niaba, wapo nao wanahusika.”
“Wapo wanaohusika katika wizara ya Mambo ya Ndani lakini kitendo cha
Zimamoto na ni wasaidizi wa Andengenye ni lazima wajitathmini,” amesema
Magufuli