Rais magufuli awatakia watanzania heri ya mwaka mpya 2020

 

 Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewatakia Watanzania wote heri ya Mwaka mpya wa 2020 na kuwaomba
waendelee kudumisha amani na upendo ili uwe mwaka wa maendeleo na ustawi
kwa Taifa.


Mhe.
Rais Magufuli ametoa salamu hizo jana  wakati akiagana na Maafisa na
Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa
cha Rubondo ambako alitembelea na kujionea vivutio vya utalii pamoja na
wananchi wa Nyabugera na Muganza aliowasalimu wakati akiwa njiani
kurejea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.

Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea salamu za heri ya Mwaka Mpya wa
2020 kutoka kwa wananchi, viongozi mbalimbali wakiwemo Marais Wastaafu,
Maaskofu na Masheikh ambao wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuongoza nchi
kwa mafanikio makubwa na wamemuelezea matarajio yao ya kufanikiwa zaidi
katika mwaka ujao.

“Mhe.
Rais wangu, Dkt. Magufuli, Bwana Yesu Asifiwe. Ninakupa hongera sana
kwa wajibu mzito ulionao. Kwa neema ya Mungu tumejaaliwa kufikia siku ya
mwisho kwa mwaka huu wa 2019. Mimi nakupongeza kwa jitihada zako nyingi
za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Ninakuombea na kukutakia Mwaka Mpya
2020 wa heri na mafanikio makubwa. Uso wa Bwana uende nawe popote
utakapokuwa”
amesema Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Frederick Shoo.

Kabla
ya kuondoka katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Mhe. Rais
Magufuli amemshukuru Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) Dkt. Allan Kijazi, Maafisa na Askari wote wa hifadhi hiyo kwa
mapokezi mazuri na juhudi kubwa zilizowezesha hifadhi hiyo kuvutia na
amewahakikishia kuwa pamoja na kutoa shilingi Bilioni 2 za ujenzi wa
kivuko cha kwenda hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo, Serikali itatoa
shilingi Milioni 200 za kuboresha barabara za hifadhi hiyo.

Baada
ya kuvuka ziwa Victoria kwa kivuko cha MV Chato, Mhe. Rais Magufuli
amekutana na wananchi wa Kasenda na kuelezea kutoridhishwa kwake na
ukusanyaji wa mapato ya soko la dagaa na samaki la Kasenda baada ya
kuelezwa kuwa makusanyo ya mapato ya soko hilo ni shilingi laki 5 kwa
siku licha kuwa soko kubwa namba 2 kwa kuuza dagaa katika ukanda wa Ziwa
Victoria.

Mhe.
Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, kufuatilia ukusanyaji
wa mapato katika soko hili na kuchukua hatua za kudhibiti mianya ya
upotevu wa mapato itakayobainika ili Halmashauri ya Wilaya ya Chato
iweze kupata fedha zitakazosaidia kutatua kero za wananchi ikiwemo
kuboresha mazingira ya soko hilo na ujenzi wa shule ya sekondari ya
Nyabugera ambayo amechangia shilingi Milioni 5.

Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chato Bw. Eliud Mwaiteleke kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya
Kasenda – Muganza yenye urefu wa kilometa 2.2 ili ijengwe kwa kiwango
cha lami kama alivyoahidi, na kwamba Serikali itatoa fedha za ujenzi wa
barabara hiyo.

Mhe.
Rais Magufuli pia amewasalimu wananchi wa Muganza, ambapo amewapongeza
kwa maendeleo yaliyopatikana katika eneo hilo na amewahakikishia kuwa
Serikali itaendelea kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma ili
iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye manufaa kwa
wananchi.

“Nchi
hii ilikuwa inaliwa sana na majizi na mpaka sasa bado wapo, namuomba
Mwenyezi Mungu aendelee kunipa uhai ili katika mwaka 2020 niendelee
kuwatumbua majizi wote na fedha tutakazopata tuzipeleke kwenye miradi ya
maendeleo kama ambavyo tumenunua ndege 11, tunajenga reli (standard
gauge), tunatoa elimu bure na mengine mengi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe.
Rais Magufuli pia amemuonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chato Bw. Eliud Mwaiteleke kwa matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na
halmashauri hiyo na ametaka dosari hizo zirekebishwe mara moja. “Nataka
ujirekebishe, wananchi hawa wanateseka sana” amesisitiza Mhe. Rais
Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato