Rais magufuli kuanza ziara dodoma kesho

ZIARA YA KIKAZI YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MKOANI DODOMA

Ndg. Waandishi wa Habari
Natumia
fursa hii kuwatangazia wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na umma wa
Tanzania kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, imempendeza kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa
wa Dodoma, Makao Makuu ya nchi, kuanzia tarehe 21 hadi 25 Novemba, 2019.

Katika
ziara yake Mkoani Dodoma, Mhe. Rais atatembelea miradi mbalimbali ya
maendeleo inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Dodoma. Vilevile, atatumia ziara
yake kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla
kupitia Mikutano kadhaa ya hadhara ambayo  hotuba hizo zitarushwa moja
kwa moja (mubashara) kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Ndg. Waandishi wa Habari

Miongoni mwa shughuli atakazofanya ni kama ifuatavyo:-

Alhamisi
Novemba 21, 2019, Mhe. Rais atakuwa ni Mgeni Rasmi katika Mahafali ya
kumi (10) ya Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM yatakayofanyika kwenye ukumbi
wa Chimwaga, Chuoni hapo.
 
Ijumaa
Novemba 22, 2019 Mhe. Rais atatembelea na kuweka mawe ya msingi kwenye
miradi ya Hospitali ya Uhuru, Wilayani Chamwino; ujenzi wa nyumba 118 za
Askari Polisi katika maeneo ya FFU Nzuguni na Medeli East; Ujenzi wa
Stendi Kuu ya mabasi iliyopo Nzuguni; na Soko Kuu linalojengwa katika
eneo la Nzuguni na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara
utakaofanyika katika stendi ya mabasi Nzuguni. 
 
Jumatatu
Novemba 25, 2019 Mhe. Rais ataweka mawe ya msingi kwenye miradi ya
ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania Kikombo; ujenzi wa
Ofisi ya Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji na Ujenzi wa jengo la
Makandarasi katika eneo la National Capital City.

Ndg. Waandishi wa Habari

Maandalizi
yote yamekamilika na Sisi wana Dodoma, kama ilivyo kwa watanzania wote,
tunaelewa fika wingi na uzito wa majukumu aliyonayo Mhe. Rais ya
kujenga Tanzania mpya na yenye matumaini makubwa kimaendeleo na ustawi
wa Jamii. Hivyo, kupata nafasi ya kufanya ziara kwenye Mkoa wa Dodoma,
licha ya majukumu hayo, ni upendeleo usiokuwa na kifani. Hivyo kwa niaba
ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe.
Rais kwa upendeleo anaotupatia daima.

Ziara
hii ya Mhe. Rais kwetu ni fursa ya kumwonesha hatua tulizofikia katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyotupatia na kupokea maelekezo ya
namna ya kusonga mbele kwa uhakika katika hatua mbalimbali za
utekelezaji wake. Aidha, atatumia ujio huu kuelekeza yale atakayoona
kuwa yatazidi kuboresha utendaji wetu na yatakayotupa shime na hamasa
zaidi ya kusonga mbele zaidi kimaendeleo. Hivyo, wananchi wa Dodoma
tujitokeze kwa wingi kuungana na Rais wetu mpendwa na hivyo, kufanikisha
ziara yake.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA!

Dkt. Binilith S. Mahenge
MKUU WA MKOA
NOVEMBA 20, 2019