Rc sanare aomba ushirikiano, aiweka gairo mguu sawa

Na, Farida saidy,Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.
Loata Ole Sanare amewataka Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Gairo
Mkoani humo kufanya kazi na watumishi wao kwa karibu, Usawa na bila
kuweka matabaka ili kuimarisha Umoja miongoni mwao.
Mhe. Ole Sanare ametoa Maagizo
hayo Oktoba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Gairo alipofika Wilayani hapo kwa lengo la kuwasalimia na kujitambulisha
akiwa njiani kutoka Dodoma kikazi.
Mhe. Sanare alipata fursa ya
kuongea na watumishi wa Halmashauri hiyo na kubainisha kuwa hadi sasa
amekwishapokea ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa wananchi na watumishi
wakieleza kuwa mambo hayako shwari ndani ya Halmashauri hiyo,  hivyo
akawataka viongozi kutoweka  matabaka katika utendaji wao wa kazi.
“wasaidie waweze kufanya kazi zao vizuri, tusije tukajaribu kuwa na matabaka ndani ya utumishi” alisema Mhe. Sanare.
Aidha, Mhe Sanare amekemea tabia
ya kutumia fedha za makusanyo ya ndani ya halmashauri kabla
hazijaingizwa kwenye Ankauti ya Benki ya Halmashauri hiyo, na kwamba huo
sio utaratibu wa Serikali, hivyo ameagiza matumizi yote ya fedha za
makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo yafanyike baada ya fedha hizo
kuingizwa kweny Ankaunti ya Benki ya Halmashauri.
“Kuanzia leo fedha zote ziingie
kwenye Ankaunti ya Halmashauri zitoke kwenye Ankaunti kwa ajili ya
matumizi”alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Sambamba na hayo Mhe. Ole Sanare
ameomba ushirikiano kutoka kwa watumishi wa Halmashauri hiyo,
kushirikiana na Ofisi yake pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa
na Wilaya ili kuondoa sintofahamu iliyopo katika Halmashauri hiyo.
“Nini hiki kinachoedelea ndani ya
Halmashauri, hatupaswi kuvumilia hata dakika moja. Mlango ulioingilia
ndio huu utatokea huo huo”.  alionya.
Amesema anajua kuna mambo ya ovyo
yanaendelea kufanyika katika Halmashauri hiyo, hata hivyo
amewahakikishia kuwa mambo hayo yapo mwishoni kuisha na kwamba itabidi
kuvumilia pale atakapolazimika kuchukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya
watumishi wa Umma wasiowajibika ipasavyo.
Pamoja na kutoa onyo hilo kwa
watumishi wanaofanya kazi ndani ya Halmashauri hiyo bado amewapongeza
watumishi ambao wanaendelea kufanya kazi zao kwa bidii, uadilifu na
uwajibikaji mkubwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa
Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Masasi Kalobelo ameungana na Mkuu
wake wa Mkoa, kutaka viongozi wa Halmashauri hiyo kusimamia kikamilifu
ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi yake.
Mhandisi Kalobelo pia amesema
usimamizi wa miradi ya maendeleo bado ni changamoto kwa Halmashauri hiyo
na kwamba ataomba kupewa taarifa ya miradi yote ikiwemo miradi yenye
changamoto katika utekelezaji wake aliyoiita Miradi chechefu ili
aifanyie kazi.
Katika hatua nyingine Mhandisi
Kalobelo ameagiza watendaji wa Halmashauri hiyo kutoa taarifa mbalimbali
za Kiserikali katika Ofisi yake kwa wakati na zilizo sahihi.
“kitu ambacho  ni kipimo cha
ufanyakazi wetu na ufanisi wetu ni utoaji wa taarifa kwa wakati na
iliyosahihi” alisema Mhandisi Kobelo.
“kwamba tunapaswa kufikia lengo,
lengo halifikiwi katikati kumekuwa na sababu lakini inawezekana sababu
zimekuwa hazitolewi kwa wakati” alisisitiza.
Aidha  Katibu Tawala huyo wa Mkoa
amewataka watumishi wa Serikali katika Wilaya hiyo na Mkoa mzima kwa
jumla kusimamia kwa ukamilifu zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
linalotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Gairo Mhe. Siriel Mchembe alimueleza Mkuu wa Mkoa mwelekeo mzuri wa
makusanyo ya ndani ya mapato ya Halmashauri hiyo kutokana na uwepo wa
machimbo ya madini ya Dhahabu ya Kilama huku akiomba mahusianao baina ya
Ofisi yake na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuboreshwa.
Nao watumishi wa Halmashauri hiyo
wamemueleza Mkuu wa Mkoa changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo
changamoto ya kukosekana kwa UMOJA miongoni mwao.
Hivyo, Wamemuomba Mkuu wa Mkoa
kuitolea ufumbuzi changamoto hiyo kwani licha ya changamoto hiyo
kuwawacheleweshea wananchi maendeleo yao lakini pia ni kikwazo kwa
watumishi wa Wilaya hiyo katika Utendaji wao wa kazi.