Arusha. Katibu tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega amefariki katika ajali ya gari leo Jumatano Februari 3, 2021 wakati akitoka mkoani humo kwenda Dodoma baada ya gari alilokuwa amepanda kugongana na basi.
Akizungumza na Mwananchi Digital mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amesema ajali hiyo imetokea eneo la Mdori Mizani.
Amesema katika ajali hiyo watu wengine wanne wamejeruhiwa ambao ni dereva wa katibu tawala huyo na wanawake watatu waliokuwa kwenye basi.
“Ni ajali mbaya kumpoteza katibu tawala na muda huu tunajiandaa kurejesha mwili Arusha bado tupo kituo cha afya hapa Magugu,” amesema.
Katibu tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega
Amesema majeruhi wanaendelea vizuri na wamehamishiwa hospitali ya Mkoa wa Manyara.B
Basilililogongana na gari la katibu tawala huyo lilikuwa linatoka Singida kwenda Arusha.
Leo asubuhi Kwitema alimwakilisha katibu mkuu wa Wizara ya Fedha, Dotto James kwenye mkutano wa wizara hiyo na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu uboreshaji wa mfumo wa kielektroniki wa malipo serikalini (GePG) uliofanyika mjini Arusha.