Rc chalamila awafukuza shule wanafunzi saba



Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ametangaza kuwafukuza Shule
wanafunzi saba wa kidato cha sita, waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za
kuchoma moto mabweni, katika Shule ya Sekondari Kwanja iliyopo Chunya
mkoani Mbeya.


Chalamila ametoa maamuzi hayo leo Oktoba 23, 2019, akiwa Shuleni hapo
wakati akitoa ripoti kuhusiana na maamuzi ya kuwatimua wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Kiwanja wa kidato cha 6 na kuwataka walipe faini ya
Shilingi laki 2 kwa kila mmoja, na faini ya Shilingi laki 5 kwa kila
aliyechoma moto mabweni.


“Leo Jumanne asubuhi nimewatimua wanafunzi wote ambao hawajalipa, na
nitaandika ripoti kwenye mamlaka kuwazuia wasifanye mitihani tena kwa
muda wa miaka 5 na kama kuna shule yeyote itawapokea itakuwa hatarini”
amesema Chalamila.


“Jinsi ya kuwafuatilia hawa wanafunzi ni ndogo sana, kwa sababu
tunawafahamu tangu walipoanzia mpaka wapo sasa na uzuri zaidi
tumewalipia ada wenyewe wala hawatusumbui kuwapata, kwa hiyo niseme tu
shule yeyote itakayowapokea itakuwa matatizoni” amesema Chalamila.

 Hivi karibuni Mkuu huyo wa Mkoa, alionekana kuwashushia bakora baadhi ya
wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kiwanja mkoani humo, wakituhumiwa
kuchoma moto mabweni ya Shule.