Rc gambo aiasa bodi ya rea kuitendea haki nafasi waliyopewa

Na Veronica Simba – ARUSHA

Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameiasa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REB), kuitendea haki nafasi waliyopewa na Mheshimiwa
Rais John Magufuli; kwa kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na weledi,
hususan katika sekta ya nishati ambayo wanaisimamia.

Gambo
ametoa wito huo leo, Oktoba 9, 2019 wakati Kamati ya Ufundi ya Bodi
hiyo, ilipomtembelea ofisini kwake, ikiwa katika ziara ya kukagua
maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, mkoani humo.

“Itumieni
nafasi mliyopewa na Rais kuhakikisha wananchi, hususan walioko
vijijini, wanapata nishati ya umeme ili waweze kuboresha maisha yao.”

Aidha,
Mkuu huyo wa Mkoa, ameishauri Bodi hiyo kushughulikia maagizo
yaliyotolewa na Rais Magufuli, kupeleka umeme katika migodi mbalimbali
ya madini ili kuwawezesha wachimbaji kuendesha kazi zao kwa tija.

“Hapa tuna Soko la Madini Karatu, nitafurahi nikisikia mmewapelekea umeme.”Katika
hatua nyingine, Gambo ameipongeza REA kwa kuwapelekea umeme wananchi wa
Wilaya ya Longido ambao awali hawakuwa kwenye Mpango, lakini kwa
maelekezo ya Wizara, walijumuishwa na tayari walikwishaanza
kuunganishiwa umeme.

Akizungumza
kwa niaba ya Ujumbe huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya REA,
Mhandisi Styden Rwebangila amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba
watafanyia kazi maelekezo yake.

Amesema,
Bodi imempa Mkandarasi NIPO Group, anayetekeleza mradi wa umeme
vijijini mkoani Arusha siku 21 kuhakikisha anasimika nguzo zote zaidi ya
1,000 zilizo chini, kuvuta nyaya pamoja na kuwanganishia umeme wananchi
wote waliolipia, na kwamba asipotekeleza hayo, hatua za kimkataba
zitachukuliwa dhidi yake.

Akitoa
takwimu za utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini, Awamu ya Tatu,
Mzunguko wa Kwanza, mkoani humo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa
REA, Mhandisi Jones Olotu amesema, mkandarasi amefikia asilimia 52 kati
ya 62.5 alizopaswa kuwa amefikia hadi sasa.

Aidha,
alibainisha kuwa, amewasha umeme katika vijiji 39 kati ya 126
anavyotakiwa kuwasha na ameunga jumla ya wateja 1,880 kati ya 5,428
anaotakiwa kuwaunga kwa Mkoa mzima wa Arusha.

Bodi inatarajiwa kufanya maamuzi dhidi ya Mkandarasi baada ya siku 21 ilizompa kuisha.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (katikati), akizungumza na Kamati ya
Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB),
ofisini kwake, Oktoba 9, 2019.