Rc mnyeti azindua barabara za kiteto

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza baada ya kuzindua mojawapo ya barabara za Wilaya ya Kiteto.
Meneja wa Wakala wa
barabara wa Mijini na Vijiji (TARURA) Wilaya ya Kiteto mhandisi Edwine
Magiri (kushoto) akizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander
Pastory Mnyeti (katikati) kuzindua mojawapo ya barabara za eneo hilo.
……………….
MKUU wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amezindua barabara za Wilaya ya Kiteto
za urefu wa kilomita 19.14 zilizotengenezwa kwa gharama ya shilingi
380,883,000.
Meneja wa wakala wa
barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kiteto mhandisi Edwine
Magiri akizungumza baada ya RC Mnyeti kuzindua barabara hizo alisema
zimefanyiwa matengenezo kwa kuanzia April 2019 hadi Julai 2019. 
Mhandisi Magiri
alisema kati ya barabara hizo kilomita 19.14 zimewekewa changarawe na
nyinginezo zimefanyiwa ukarabati wa kawaida. 
Alisema katika ujenzi wa kilomita hizo za barabara hizo kumewekewa na kujengewa kalvati 22 na pia kumejengwa madrifti mawili. 
“Kazi zimefanyika kwa
wakati na kiwango kinachotakiwa ikiwemo vipimo kwani tulisimamia ujenzi
ipasavyo wakati wa shughuli hiyo,” alisema mhandisi Magiri. 
Mkuu wa mkoa wa
Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza wakati akizindua mojawapo
kati ya barabara hizo aliwapongeza Tarura Kiteto kwa namna
walivyotengeneza barabara hizo. 
Hata hivyo, Mnyeti
alitoa wito kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara kuwa na tabia
ya kusafisha mazingira ili ziwe safi kwa kuondoa uchafu. 
“Kuna ule utaratibu
wa kufanya usafi kila mwisho wa mwezi, tumieni nafasi hiyo kwa
kuhakikisha mnaondoa uchafu uliopo pembezoni hasa katika mitaro,”
alisema Mnyeti. 
Pia, Mnyeti
aliipongeza Tarura na wakala wa barabara za nchini (Tanroads) mkoani
humo kwa namna wanavyotengeneza barabara na kuzikarabati pindi kukitokea
matatizo. 
“Ukipita Manyara
unakuta barabara zake zinapitika bila shida hongereni kwa hilo kwani
ukipita sehemu nyingine unaona changamoto kwa wenzetu namna barabara zao
zilivyo,” alisema Mnyeti.