Rrc morogoro “achochea moto” wa majaliwa, aagiza diwani afikishwe mahakamani

Na, Mwandishe wetu – Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole
Sanare ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ngazi
ya Mkoa na Wilaya kuwahoji watumishi wawili, Afisa Manunuzi na Mhandisi
wa Majengo wa Wilaya ya Ulanga kwa tuhuma ya kutosimamia ipasavyo fedha
zaidi ya shilingi 400 Mil. zilizoletwa Wilayani humo kwa ajili ya
kuboresha Hospitali ya Wilaya hiyo.

Ole Sanare ametoa agizo hilo
Oktoba 30 mwaka huu alipotembelea ujenzi wa jengo litakalotumika kama
Wodi ya akinamama ikiwa ni moja kati ya majengo manne yaliyopelekewa
fedha hizo kwa lengo la kuboresha huduma ya Afya katika Hospitali ya
Wilaya ya Ulanga.

Akiambatana na Wajumbe wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa huyo alifika kukagua ujenzi
wa jengo hilo ambalo liko katika hatua ya upauaji na kukuta mbao
zinazotumika kuezeka hazina kiwango na hazijawekewa dawa ya kuzuia
wadudu wahalibifu (Treated). Baada ya mahojiano ya muda ikaonekana kuna
kila dalili ya mbazo zinazotumika katika jingo hilo hazikidhi vigezo vya
BOQ hivyo kuagiza TAKUKURU kuwachunguza watumishi hao,

“hakuna kucheza, fedha zimeletwa kwa ajili ya kuwahudumia watu
wa Ulanga, usihangaike kutemba na hizo fedha, utatapika” alionya Ole
Sanare.

Aidha, Mhe. Ole Sanare amesema
hata kama itadhibitika hawakutumia hizo fedha za mradi huo kwa maslahi
yao binafsi lakini kama wataalamu bado wana kosa la kutosimamia ipasavyo
matumizi ya fedha hiyo ya Serikali hivyo ni lazima wawajibike.
“Chunguzeni pelekeni mahakamani,Mkurugenzi wakiwepo mahakamani
anzeni process hatua nyingine ziandaliwe hatua za kinidhamu ukitoka
unalo”

Mkuu wa Mkoa pia anatumia fursa hiyo ya kujitambulisha
kufuatilia Maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Kassim Majaliwa aliyoyatoa wakati wa ziata yake Mkoani Morogoro
Mwezi Septemba mwaka huu.

Amesema kwa kiasi fulani baadhi ya
maagizo yaliyotolewa na kiongozi huyo yametekelezwa lakini akataka
kuongeza kasi kwa yale ambayo hayajatekelezwa huku akiagiza watumishi
nane wanaotuhumiwa kufanya ubadhilifu wa fedha za Halmashauri hiyo zaidi
ya shilingi 1.4 Bil, kufikishwa mahakamani haraka na wale wanaojaribu
kutoroka wakamatwe mara moja.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa
Mkoa ameagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kumfikisha mahakamani Diwani
Kesy Mponda Wilayani humo anayetuhumiwa kukaidi kurudisha fedha za
Serikali alizochukua kwa ajili ya kwenda kwenye ziara ya majifunzo ya
Kilimo kwenye Maonesho ya Nanenane Mjini Morogoro mwaka huu 2019 pamoja
na Madiwani wenzake lakini alishindwa kushiriki mafunzo hayo.

Imeelezwa kuwa katika Halmashauri
hiyo kulikuwa na jumla ya Madiwani watano ambao walikuwa wanadaiwa fedha
za Serikali na baada ya kutaarifiwa kuzirudisha fedha hizo madiwani
wanne walitii agizo hilo na kuzirudisha isipokuwa yeye jambo
lililomlazimu Mkuu wa Mkoa kuagiza Diwani huyo kufikishwa mahakamani
Oktoba 31, mwaka huu.

Mwenyekeiti wa Halmashauri hiyo
Furaha Lilongeli amethibitisha kuwepo kwa Sakata hilo na kwamba yeye
anachojua Diwani huyo siku hiyo alipashwa kuwepo kwenye ziara hiyo
lakini alishindwa kutokana na dharura na kuuguliwa na mtoto wake.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa
Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobero kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya
ya Ulanga ili amkaribishe Mkuu wa Mkoa kuongea na watumishi wa Wilaya
hiyo alieleza kwa ufupi lengo la ziara hiyo huku akiwataka watumishi
wote wa Mkoa wa Morogoro kufanya kazi zao kwa kufuata misingi ya
Utumishi na Kanuni zake.

Aidha, Mhandisi Kalobelo alieleza
uwepo wa tatizo sugu karibu Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro
kutofanyia kazi ushauri unaotolewa na Wadhibiti Ubora wa Elimu katika
maeneo yao na kupelekea Kushuka kwa Elimu ndani ya Mkoa huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Jonas Malosa anampongeza
Mkuu wa Mkoa Ole Sanare kwa kufuatilia kwa karibu matumizi mabaya ya
fedha za Serikali bila kujali nafasi ya mtu aliyo nayo.