Rc tabora awataka tra kutumia tehama kujenga mazingira rafiki na mlipa kodi

NA TIGANYA VINCENT
WATUMISHI
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wametakiwa kutumia Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kujenga mazingira rafiki kwa mlipa kodi
ili aweze kutumia mifumo hiyo katika ulipaji kodi na hivyo kuongeza
mapato ya Serikali.


Kauli
hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati
akifunga mafunzo ya siku sita ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika
utendaji kazi kwa  Watendaji wa TRA wa Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora
wanaohusika na ukusanyaji wa mapato.

Alisema
ni vema wakatumia elimu waliyopata kuboresha utoaji wa huduma ambap
watamfanya  Mlipa kodi aweze kutumia muda mfupi na gharama nafuu katika
ulipaji kodi jambo ambalo litasaidia kuongeza mapato ya Serikali.

Aidha
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Wafanyakazi hao wa TRA kuendelea kutoa
elimu kwa wananchi ili wajue wajibu wao katika kulipa kodi kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa.

Naye
Meneja wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Lazaro Swai alisema lengo la mafunzo
hayo ilikuwa ni  kuwaongezea ujuzi watumishi ili waweze kufanya kazi zao
kwa ufanisi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.

Alisema
kuwa elimu waliyopata itawasaidia kuwawezesha walipa kodi kuweza kulipa
Kodi katika mazingira jirani ikiwemo Ofisi kwao au kwa Wakala badala ya
kusafiri hadi TRA na kutumia muda na gharama za usafiri.

Swai
alisema Mifumo ikitumika vizuri itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato
ya Serikali na hivyo kuwa na fedha nyingi za kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

Kwa
upande wa Meneja wa TRA Mkoa wa Tabora Thoams Masese alisema mafunzo
yaliyotolewa yatawasaidia watumishi wa TRA katika kuwasaidia walipa kodi
ili waweze kulipa katika mazingira ambayo wataona ni rahisi kwao na
kuwapunguzia usumbufu na hivyo kuwezesha kuongeza makusanyo ya Serikali.