Serikali kulipa mil 315.1 za wakulima wa muzia amcos

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Rukwa
 

Serikali
imetangaza dhamira yake ya kuwalipa wakulima 156 wa mahindi jumla ya
Shilingi 315,118,510 kutokana na kuzulumiwa na mwenyekiti wa Chama cha
Ushirika Ndg Linus Kalandamwazye.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo tarehe 13 Octoba
2019 wakati akizungumza na wanachama wa Muzia Amcos Wilayani Kalambo
wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.
Malipo hayo yatawahusu wakulima wa Tarafa ya Mwimbi yenye kata nne
ambazo ni Mambwe Kenya, Ulumi, Mkombo na Mwazye kutokana na kupima
mahindi yao zaidi ya Tani 622.679 kwenye Chama cha Muzia Amcos
kilichopewa uwakala na serikali wa kununua mazao kwa wakulima tarehe 8
Agosti 2017 kwa makubaliano ya kulipwa ndani ya wiki tatu kutoka tarehe
ya kupimwa lakini hawakulipwa mpaka sasa.
“Kesi ikiwa mahakamani serikali haiwezi kuingilia badala yake wakati
tunaendelea na kesi hiyo ninaziagiza taasisi zangu tatu kuchanga fedha
kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao” Alikaririwa Mhe Hasunga
Alisema wanaotakiwa kuchanga fedha hizo kwanza ni Wizara ya Kilimo kwa
kushindwa kulishughulikia jambo hilo kwa wakati ili wakulima hao waweze
kulipwa fedha zao.
Ameiagiza pia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuchanga fedha hizo kwani
wao ndio wasimamizi wa Vyama vya Ushirika lakini kwa kipindi chote
wameshindwa kushughulikia changamoto hiyo ya wakulima.
Kadhalika, Mhe Hasunga Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuchangia fedha hizo.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya
tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli haina dhamira ya
kuwadunisha na kuwafedhehesha wananchi badala yake imejipambanua
kuwanufaisha wakulima katika kilimo.
Alisema kuwa serikali imeamua kuwalipa fedha hizo wakulima ili kuendelea
na uzalishaji bora wa mazao ya kilimo lakini kesi itakapomalizika
serikali itazidai fedha hizo.
Mhe Hasunga amemuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Rukwa kupanga vizuri
madai ya wakulima hao huku akisisitiza kutoingizwa majina mapya (Majina
Hewa) yasiyohusika na madai ya fedha hizo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe Joachim Wangabo amempongeza Waziri wa
Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwa kukubali kulivalia njuga jambo hilo
kwa kuwalipa fedha hizo wakulima kwani kufanya hivyo kutarahisisha
wakulima hao kuendelea na uzalishaji wa mazao katika msimu wa kilimo wa
mwaka 2019/2020.
Amesema kuwa maamuzi hayo ya wizara kuamua kuwalipa wakulima huku
taratibu zingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua
Mwenyekiti huyo zikiwa zinaendelea zimeibua ari na nguvu mpya katika
kilimo.
Awali, akisoma taarifa ya malalamiko ya kutapeliwa fedha hizo katibu wa
chama cha MUZIA AMCOS Ndg Geofrey Mbati amesema kuwa pamoja na kupeleka
malalamiko katika maeneo mengi lakini ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa kwa ushirikiano wa karibu katika kipindi chote cha kutafuta
muarobaini wa malipo ya wakulima.
Alisema kuwa miongoni mwa maoni ya wakulima ilikuwa ni ombi la kupatiwa
fedha hizo kwa ajili ya kuwanusuru kutokana na kadhia hiyo ya muda mrefu
iliyopelekea kushindwa kulipa ada za wanafunzi shuleni, kushindwa
kuwekeza tena kwenye kilimo pamoja na kushindwa kumudu gharama za maisha
hali iliyopelekea kuishi maisha ya kifukara.